'
Thursday, August 15, 2013
YANGA USO KWA USO NA AZAM TV
UONGOZI wa klabu ya Yanga na kituo cha televisheni cha Azam umekubaliana kukaa meza moja kwa ajili ya kujadili bifu lililojitokeza katika kupitia mkataba wa awali wa kuonyesha mechi za ligi kuu laivu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu,Walace Karia alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa kikao cha pamoja kati ya pande hizo na
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Karia alisema kikao hicho kilifanyika jana katika ofisi za wizara hiyo kwa lengo la kutafuta mwafaka wa hali ya kutokuelewana iliyojitokeza kati ya uongozi wa Yanga na Azam TV.
Alisema katika kikao hicho, pande hizo mbili zimetakiwa kukutana pamoja na wanasheria wao ili waweze kuboresha makubaliano ya awali katika mkataba huo.
Karia alisema katika kikao hicho,Yanga iliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti,Clement Sanga,Kaimu Katibu Mkuu,Lawrence Mwalusako na mwanasheria wao.
TFF iliwakilishwa na rais wake, Leodegar Tenga, Katibu Mkuu, Angetile Osiah wakati Kamati ya Ligi iliwakilishwa na Karia na mwanasheria wao, Damas Ndumbaro. Azam TV iliwakilishwa na mkurugenzi wao, Abubakar Bakhresa na mwanasheria wa kampuni hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment