KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, August 24, 2013

LIGI KUU BARA KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO



Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua
vumbi leo (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti huku mabingwa
watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Ashanti United
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi
kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT itaikaribisha
Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini
Arusha.

Mgambo Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko chini ya
Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati
Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini
Tabora.

Mbeya City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting ikiialika
Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya hapo ligi
itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Gambia na
Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul. VPL
itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.

TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUANZA MZUNGUKO WA NNE
Tiketi za elektroniki zitaanza kutumika katika mzunguko wa nne wa Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) utakaoanza Septemba 18 mwaka huu. Tayari benki ya CRDB
ambayo ndiyo ilishinda tenda hiyo imeshakamilisha ufungaji wa vifaa kwa ajili ya
matumizi ya tiketi hizo katika viwanja vyote.

Hivi sasa Serikali ambayo ndiyo inamiliki Uwanja wa Taifa, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) pamoja na CRDB zinashughulikia mfumo wa tiketi hizo kwenye
uwanja huo ambao ndiyo ulikuwa haujakamilika kwa matumizi katika upande huo.

Mfumo (system) iliyoko kwenye uwanja huo inapishana na ule utakaotumiwa na
CRDB, hivyo pande husika zinashughulikia suala hilo ili mifumo hiyo iweze kuingilia.

Pia mashine za kuchapia (printer) kwa ajili ya tiketi ambazo CRDB wameziagiza
kutoka nje ya nchi zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.

Hivi sasa CRDB inashughulikia ufungaji wa vifaa vya matumizi ya tiketi za elektroniki
iwemo turnstiles kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao mwanzoni hakuwemo
kwenye mpango huo kutokana na Mkoa wa Tabora kutokuwa na timu ya Ligi Kuu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment