HATIMAYE mshambuliaji Hamisi Kiiza ametia saini mkataba wa kuendelea kuitumia Yanga kwa miaka miwili.
Kiiza alitia saini mkataba huo juzi mbele ya mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Mussa Katabalo.
Uamuzi wa Kiiza kumwaga wino Yanga umekuja baada ya mchezaji huyo kudengua kufanya hivyo zaidi ya mara tano.
Kiiza aliupa uongozi wa Yanga masharti ya kutaka alipwe sh. milioni 40 taslim za usajili, lakini uongozi wa klabu hiyo ulikuwa ukitaka kumpa malipo hayo kwa awamu mbili.
Hali hiyo ilisababisha Kiiza atake kurudi katika klabu yake ya zamani ya URA ya Uganda huku Yanga ikimwita Dar es Salaam mara nne kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo, lakini bila mafanikio.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Kiiza amekubali kumwaga wino baada ya uongozi kukubali kumpatia fedha zote alizokuwa akitaka kulipwa.
Kiiza anakuwa mchezaji wa nne wa kigeni kusajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa ligi. Wengine ni Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Didier Kavumbagu.
Yanga bado inayo nafasi moja ya mchezaji wa kigeni na imekuwa ikimuwinda kwa udi na uvumba mshambuliaji Moses Oloya wa Uganda anayecheza soka ya kulipwa nchini Vietnam.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza kulia akisaini Mkataba wa kuendelea kuichezea Yanga SC kwa miaka miwili zaidi. Anayemshuhudia kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Mussa Katabaro
No comments:
Post a Comment