KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 4, 2013

SALUM ZAHORO: MUZIKI HAUJANISAIDIA CHOCHOTE


KWA mashabiki wa muziki wa dansi chini wa 'zilipendwa', jina la Salum Zahoro linawakumbusha enzi za miaka ya 1960 na 1970 wakati bendi ya Kiko Kids iliyokuwa na maskani yake Tabora ilipokuwa ikitingisha nchi.

Vibao kama vile Wamtetea bure, Sili Sishibi, Umeniasi mpenzi, Mpenzi wangu wanionea, Tanganyika na Uhuru na Bahati ni miongoni mwa vilivyoipatia sifa kubwa bendi hiyo, vikiwa ni utunzi wake Zahoro.

Pamoja na kupiga muziki kwa miaka mingi akiwa na bendi hiyo, Zahoro hakuweza kunufaika lolote kimaisha zaidi ya kupata sifa na umaarufu.

Si kwamba hakujitahidi kutumia kipaji chake kuinua maisha yake. La hasha! Alirekodi nyimbo zake nyingi katika studio za Asanandi iliyokuwepo Mombasa, Phillips na Daudia zilizokuwepo Nairobi nchini Kenya, lakini fedha alizopata hazikulingana na jasho lake.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii hivi karibuni nyumbani kwake Buguruni mjini Dar es Salaam, Zahoro alisema kutokuwepo kwa sheria ya hatimiliki ni sababu kubwa iliyowafanya wanamuziki wa enzi zake kutonufaika lolote kutokana na muziki.

"Kungekuwepo na sheria hiyo tangu enzi zetu, bila shaka hivi sasa ningekuwa na maisha mazuri, ningemiliki nyumba na gari. Lakini maisha yetu sisi wanamuziki wa zamani wa Tanzania ni duni na hata hatima zetu ni za wasiwasi,"alisema.

Zahoro (77) alisema kujiunga kwake na bendi ya Shikamoo Jazz, iliyoanzishwa takriban miaka sita iliyopita, angalau kumemwezesha kuyamudu vyema maisha, tofauti na alipokuwa hana bendi, ambapo maisha yake yalikuwa ya kubahatisha.

Bendi hii ilianzishwa na taasisi ya Helpage International, iliyokuwa na makao makuu yake nchini Uingereza, ambayo ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wazee. Taasisi hii ndiyo iliyoipeleka bendi hii kufanya maonyesho mara kadhaa katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwemo Uingereza.

Zahoro, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi mkuu wa bendi hiyo, alisema angalau ziara hizo zilimwezesha kufunguka macho kwa kubahatika kutembelea nchi za Ulaya na kupata pesa zilizomwezesha kununua vitu mbalimbali vya ukumbusho.

Kwa sasa, bendi ya Shikamoo Jazz imekuwa ikifanya maonyesho yake katika kumbi mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam bila kuwalipisha viingilio mashabiki wake. Bendi hiyo kama zilivyo nyingine kadhaa, inalipwa kutokana na makubaliano kati yake na mmiliki wa ukumbi (baa).

"Angalau bendi hii imeniwezesha mimi na wenzangu kupata fedha za kutuwezesha kuyamudu maisha yetu, japokuwa haziendani na kiwango cha kazi tunayoifanya,"alisema.

Akizungumzia hali ya muziki ilivyo hivi sasa hapa nchini, Zahoro alisema kiupigaji imepanda kutokana na kuingia kwa teknolojia mpya na za kisasa. Hata hivyo, alisema bado maisha ya baadhi ya wanamuziki, hasa wanaopiga muziki wa dansi ni duni.

Alisema muziki wa wakati wao ulikuwa mzuri kwa enzi zao japokuwa vyombo vilikuwa vichache na kuongeza kuwa, muziki wa sasa ni mzuri kwa wakati huu kutokana na kuongezewa ala nyingi.

Hata hivyo, Zahoro alisema nyimbo za zamani zimeendelea kuwa na mvuto ikilinganishwa na za wasanii wa muziki wa kizazi kipya kwa sababu wanamuziki wa zamani waliumiza vichwa vyao katika kutunga nyimbo zenye mashairi yenye mvuto, mpangilio wa ala na sauti.

"Mashairi ya nyimbo za zamani yanaweza kudumu hata kwa miaka 50 ijayo bila kupoteza ladha na hamu ya kuyasikiliza,"alisema.

Zahoro alisema kufa kwa bendi nyingi za zamani kulichangiwa na uchakavu wa vyombo kwa vile nyingi zilikuwa zikimilikiwa na watu binafsi, ambao hawakuwa na uwezo wa kununua vyombo vipya.

Mwanamuziki huyo mkongwe alieleza kusikitishwa kwake na utaratibu wa sasa wa vituo vingi vya redio na televisheni kutopiga nyimbo za zamani za muziki wa dansi, badala yake vimekuwa vikitoa nafasi hiyo zaidi kwa nyimbo za wasanii wa kizazi kipya.

"Nahisi kuna kampeni za kuua muziki wa dansi wa zamani ili kutoa nafasi kwa muziki wa kizazi kipya kutawala,"alisema.

Kwa mtazamo wake, Zahoro alisema muziki wa kizazi kipya hauna mvuto kwa vile una mapungufu mengi na umekuwa ukikuzwa bila ya sababu za msingi. Aliyataja baadhi ya mapungufu hayo kuwa ni kutengenezwa kwa njia ya kompyuta hivyo kukosekana kwa ala za muziki, mpangilio mzuri wa sauti na pia kutokuwepo kwa vionjo vingi vyenye mvuto.

Alisema muziki wa kizazi kipya hauna mpangilio kwa vile mwanzo hadi mwisho vyombo vinapigwa kwa staili moja. Alisema kasoro hizo zinaweza kuufanya muziki huo ushindwe kudumu kwa miaka mingi.

Zahoro alisema baadhi ya wasanii wa muziki huo wamekuwa wakitunga mashairi ya kuvutia, lakini nyimbo za wengine zimejaa lugha ya maudhi ikiwa ni pamoja na kushabikia uvutaji bangi, dawa za kulevya na vitendo vya ngono.

Mwanamuziki huyo mkongwe alisema kutokuwepo kwa maendeleo makubwa kwa wanamuziki wa zamani nchini, kumetokana na viongozi wanaohusika kusimamia masuala ya sanaa na utamaduni kushindwa kuwasaidia katika kutatua matatizo yao.

Mkongwe huyo alisema matatizo ya wanamuziki yanaeleweka wazi, lakini viongozi wa kisiasa wamekuwa wakiyafumbia macho japokuwa baadhi yao ni mashabiki wakubwa wa muziki.

Zahoro alisema licha ya Shikamoo Jazz kuundwa na wanamuziki wengi wenye umri mkubwa, bado wana uwezo wa kupiga muziki kwa kiwango kilekile, lakini wanashindwa kurekodi nyimbo zao mpya studio na pia kutengeneza video za nyimbo zao kutokana na gharama kuwa kubwa.

Mkongwe huyo wa muziki alizaliwa 1937 mkoani Tabora. Alisoma katika shule ya msingi ya White Fathers ya Tabora kuanzia 1944 hadi 1948 alipokatishwa masomo na  kupelekwa kusoma kuraani.

Alianza muziki tangu 1953 akiwa Kiko Kids, ambayo baadaye alikuwa kiongozi wake mkuu. Awali alikuwa akipiga tumba, lakini baadaye alijifunza kupiga gita la solo na kuimba.

Kiko Kids ilikufa kifo cha kawaida 1972 baada ya wanamuziki kadhaa kuondoka. Zahoro alijitahidi kuifufua kwa kuwapa mafunzo wanamuziki wapya, lakini ilipofika 1984, alipatwa na matatizo ya kifamilia yaliyomfanya aachane kabisa na muziki.

Aliamua kurejea tena katika muziki mwanzoni mwa 1990 baada ya kuundwa kwa bendi ya Shikamoo Jazz na hadi sasa ni mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo, akiwa kiongozi, mwimbaji na mpiga gita la solo.

2 comments:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. Hakika nakukubali sana kaka haswa kibao chenu cha Wamtetea bure,wimbo huu ulichezwa kipindi cha Sunday special ITV. jumapili ya tar. 07/02/2021, hakika bado kinavutia mno, naupenda mno muziki wa zamani...

    ReplyDelete