KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 28, 2013

SERIKALI YAVALIA NJUGA WIZI WA KAZI ZA WASANII


NA HAMIS SHIMYE, DODOMA

SERIKALI imesema imeshaunda tume ambayo imeazimia kuhakikisha inatatua tatizo la usambazaji wa nyimbo za msanii katika simu za mkononi.

Imesema maazimio ya tume hiyo ni kukiagiza Chama cha Hati Miliki Tanzania (COSOTA), kuzichukulia hatua kampuni za simu za mkononi nchini, ambazo zinawalipa wasanii chini ya kiwango kilichowekwa kisheria na chama hicho.

Hayo yalisemwa jana bungeni mjini hapa na Naibu Waziri wa Teknolojia, Sayansi na Mawasiliano, Januari Makamba, alipokuwa akijibu swali Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliyetaka kujua ni lini serikali itatunga kanuni za kuweka wazi mapato ya kazi za wasanii kwa kampuni za simu.

Alisema serikali inatambua changamboto mbalimbali anazokutana nazo msanii ndiyo sabau iko nao bega kwa bega kuhakikisha inatatua matatizo yao, hasa katika suala la usambazaji wa kazi za wasanii kupitia simu za mkononi.

"Wizara ilikutana na wadau na kuunda kamati iliyoshirikisha Wizara ya Viwanda na Biashara, COSOTA, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kampuni za simu na wawakilishi wa wasanii. Lengo lilikuwa ni kupata uvumbuzi wa tatizo,''alisema Makamba.

Makamba, alisema tume hiyo iliamua kutekeleza mambo mbali mbali ikiwemo malipo ya msanii yawe siyo chini ya kiwango kinachotajwa kwenye sheria ya COSOTA na isiwe kwa mawakala ili kuondoa dhuluma kwa wasanii.

Alisema pia tume hiyo, imepanga kuweka utaratibu wa kufanyia marekebisho sheria za COSOTA, BASATA na TCRA ili ziwe pamoja na kuondoa mwingiliano wa kimajukumu katika utekelezaji na uondoaji wa dhuluma kwa wasanii.

“Wizara yangu inaendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya, pia Wizara ya Viwanda na Biashara iko kwenye mchakato wa kuweka utaratibu wa wazi na haki wa kuwezesha wasanii kunufaika na kazi zao zinapopigwa kwenye radio na televisheni,” alisema Makamba.

Hata hivyo, Makamba alisema hakuna taarifa za pato ghafi lililotokana na biashara ya kuuza milio ya simu kwa kuwa mauzo ya kampuni za simu hutokana na huduma mbalimbali kama ujumbe mfupi,  M Pesa, vifurushi vya 'Internet' ambayo huchanganywa kama pato la jumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini-CHADEMA, Joseph Mbilinyi, alisema serikali ifanye kila linalowezekana kuwasaidia wasanii na kuiomba iunde tume huru itakayosaidia kuondoa tatizo la wizi wa kazi zao.

Makamba alisema Rais Jakaya Kikwete na serikali yake wana dhamira ya kusaidia wasanii ndiyo maana ilitoa kiasi sh. milioni 16 kwa ajili ya kufanyika kwa utafiti wa wizi wa kazi za wasanii. Utafiti huo ulifanywa na Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam (UDSM).

No comments:

Post a Comment