KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 14, 2013

YANGA, AZAM PRESHA JUU, ZINAKUTANA KESHOKUTWA DAR KUWANIA NGAO YA JAMII

MABINGWA wa soka wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga keshokutwa wanatarajiwa kushuka dimbani kukipiga na washindi wa pili wa ligi hiyo mwaka jana, Azam katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, inatarajiwa kuwa kali na ngumu kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Kwa kawaida, mechi hiyo ni ya ufunguzi wa pazia la ligi kuu na huchezwa kila mwaka kwa kuzikutanisha bingwa wa msimu uliopita na mshindi wa pili.

Msimu uliopita, Azam iliwania tuzo hiyo dhidi ya Simba na kuchapwa mabao 3-2 baada ya kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Katika mechi za ligi ya msimu uliopita, Yanga iliitambia Azam kwa kuifunga mechi zote mbili. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Novemba 2 mwaka jana, Yanga iliichapa Azam mabao 2-0 na katika mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa Aprili 10 mwaka huu, iliibuka tena na ushindi wa bao 1-0.

Kikosi cha Azam kitakachoshuka dimbani keshokutwa hakitakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na timu hiyo kutosajili nyota wapya msimu huu zaidi ya kuwapandisha wachezaji wake wanne kutoka kikosi cha pili.

Kwa upande wa Yanga, nayo haitakuwa na mabadiliko makubwa kwa vile wachezaji wake wengi walikuwepo msimu uliopita. Wachezaji pekee wapya wa kikosi cha kwanza ni kiungo Bakari Masoud na mshambuliaji Hussein Javu.

Katika kujiandaa kwa mechi hiyo, Yanga imecheza mechi tatu za kirafiki za kujipima nguvu. Katika mechi hizo, iliicharaza Mtibwa Sugar mabao 3-1, iliinyuka SC Villa ya Uganda mabao 4-1 kabla ya kuichapa 3 Pillers ya Nigeria bao 1-0. Mechi zote hizo zilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam imefanya maandalizi ya mechi hiyo kwa kwenda kuweka kambi nchini Afrika Kusini, ambako ilicheza mechi nne za kirafiki za kimataifa dhidi ya vigogo vya soka vya nchi hiyo.

Katika mechi yake ya kwanza, ilichapwa mabao 3-0 na Kaizer Chiefs, ilishinda bao
1-0 dhidi ya Mamelodi Sundown, ikafungwa mabao 2-1 na Orlando Pirates na kuhitimisha ziara yake kwa kipigo cha  bao 1-0 kutoka kwa Moroka Swallows.

Azam inakuwa timu ya nne kucheza mechi ya kuwania Ngao ya Jamii. Timu zingine zilizowahi kucheza mechi hiyo ni Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.

Msimu wa 2009/2010, Simba ilicheza na Yanga na kuchapwa mabao 2-1, msimu wa 2010/2011, Yanga ilicheza na Simba na kuibuka na ushindi wa penalti 3-1 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa suluhu na msimu wa 2011/2012, Simba iliichapa Yanga mabao 2-0.

Akizungumzia mechi hiyo wiki hii, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts alisema kikosi chake kimezidi kuimarika baada ya kuongezeka kwa Javu, ambaye amemuelezea kuwa ni aina ya mshambuliaji aliyekuwa akimuhitaji.

Brandts alisema kwa sasa Yanga imeimarika kwenye kila idara, ikiwa na wachezaji zaidi ya wawili katika kila namba na kwamba ushindi wa namba kwenye kikosi cha kwanza umekuwa mkubwa.

Kocha huyo kutoka Uholanzi alisema, matumaini ya timu yake kutetea ubingwa wa ligi kuu msimu huu ni makubwa, ikiwa ni pamoja na kutoa vipigo kwa wapinzani wao wakati wa ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.

Tegemeo kubwa la kocha huyo litakuwa kwa washambuliaji wake, Javu, Mrisho Ngasa, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Saidi Bahanuzi na Hamisi Kiiza, aliyeanza mazoezi juzi baada ya kumalizana na uongozi katika masuala ya mkataba mpya.

Safu ya ulinzi ya mabingwa hao inatarajiwa kuundwa na kipa Ally Mustafa 'Barthez' na  mabeki Juma Abdul, David Luhende, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kevin Yondan na Rajabu Zahir wakati safu ya kiungo itaundwa na Athumani Iddi 'Chuji', Bakari Masoud, Salum Telela, Frank Domayo na Haruna Niyonzima.

Kocha Mkuu wa Azam, John Stewart Hall alisema kupitia blogu ya Bin Zubery akiwa Afrika Kusini kuwa, hawakwenda huko kujiandaa kwa michuano ya ligi kuu pekee, bali pia michuano ya Kombe la Shirikisho.

Alisema ziara yao hiyo imewawezesha wachezaji wake kujiandaa vyema dhidi ya mechi yao na Yanga keshokutwa na mechi ya ufunguzi wa ligi wiki ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Stewart alisema licha ya timu yake kufungwa na Yanga katika mechi zote mbili za ligi kuu msimu uliopita, anajivunia rekodi yake ya kuifunga Yanga mara nne msimu uliotangulia.

"Kabla sijaondoka Azam, niliifunga Yanga mara nne. Tuliifunga 1-0, 2-0, 3-1 na 3-0. Hatufikirii Yanga inatuzidi chochote. Tuko tayari kuwafunga. Tatizo kubwa tunapocheza na Yanga ni waamuzi,"alisema kocha huyo.

“Nina wasiwasi na waamuzi, tena sana. Mara ya mwisho tulipocheza na Yanga, walitufunga 1-0, lakini refa alitunyima penalti na akakataa bao letu lililofungwa na John Bocco,”alisema kocha huyo raia wa Uingereza.

“Imekuwa kawaida unapocheza na Simba SC au Yanga, marefa wanakuwa upande mwingine. Sasa kama na kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itajirudia hivyo, itakuwa mbaya. Naomba marefa watakaopangwa wachezeshe kwa haki,”alisema Stewart.

Stewart alisema anaamini timu yake imenufaika na kambi ya Afrika Kusini na inaweza kuwapa burudani nzuri wapenzi wa soka wa Tanzania wakati wa mechi za ligi na michuano ya kimataifa.
Tegemeo kubwa la kocha huyo litakuwa kwa washambuliaji wake, John Bocco, Gaudence Mwaikimba, Kipre Tchetche, Khamis Mcha, Seif Abdalla na Mudathir Yahya.

Safu ya ulinzi ya timu hiyo inaundwa na makipa Mwadin Ally na Aishi Manula, mabeki ni Erasto Nyoni, Joackins Atudo, Waziri Salum, Samih Hajji Nuhu, Said Mourad, David Mwantika na Aggrey Morris wakati safu ya kiungo inaundwa na Jabir Azizi, Kipre Balou, Himid Mao na Ibrahim Mwaipopo.

No comments:

Post a Comment