Banana Zorro
Barnaba Elias
Pauline Zongo
Muziki huu ulipachikwa jina la kizazi kipya kutokana na kupigwa zaidi na vijana ambao hawana elimu ya muziki au utaalamu wa kutumua ala za muziki. Ni muziki unaotengenezwa studio kwa kutumia kompyuta yenye programu maalumu ya kutengeneza midundo ya ala mbalimbali za muziki.
Asili ya muziki wa kizazi kipya ni barani Ulaya, ambako baadhi ya wasanii kwa kukwepa gharama za kurekodi nyimbo kwa kutumia ala za muziki, waliamua kutumia kompyuta. Vijana wa Kitanzania waliiga mtindo huo na kuufanya muziki huo uwe maarufu kuliko mitindo mingine.
Kazi kubwa inayofanywa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya ni kutunga mashairi na kwenda kwa mtayarishaji wa muziki, ambaye hutengeneza mipigo ya ala mbalimbali kwa kutumia kompyuta.
Wakati mwingine, watayarishaji wa muziki hutengeneza mipigo ya wimbo na kuwapatia wasanii ili wautengenezee mashairi na kuimba.
Muziki wa kizazi kipya hupigwa na kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop (muziki wa kufokafoka), R&B (muziki laini wenye kuchombeza) na Zouk na unapendwa zaidi na vijana. Uliingia nchini miaka ya mwanzoni mwa 1990 muasisi akiwa Saleh Jabir, ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi.
Saleh aliutambulisha muziki huo kwa kufanya maonyesho kwenye kumbi za burudani za mjini Dar es Salaam. Alitumia CD kupiga midundo ya muziki na yeye kushika kipaza sauti na kuimba. Alikuwa na uwezo wa kutunga mashairi yanayoelezea matukio mbalimbali yanayotokea katika jamii.
Kwa sasa yapo mabadiliko makubwa katika muziki huo kutokana na wasanii kutunga nyimbo zinazosisimua na kuamsha hisia, zikielezea masuala mbalimbali. Zipo nyimbo zinazozungumzia mapenzi, ukahaba, wizi, utumiaji wa dawa za kulevya, utumiaji mbaya wa madaraka na siasa.
Muziki huu ni tofauti na uliozoeleka wa dansi, ambao wanamuziki hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake.
Kutokana na muziki huo kuwa na mashabiki wengi, baadhi ya wasanii wanaamini utadumu kwa muda mrefu, kama ilivyo kwa nyimbo za muziki wa dansi.
Selemani Msindi, maarufu Afande Sele, anasema wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya wanapenda kutengeneza nyimbo kwa kutumia kompyuta kutokana na gharama kubwa za kuwakodi wapiga ala za muziki.
“Dunia hivi sasa ni kama kijiji. Muziki wa kizazi kipya ni matokeo ya mabadiliko yanayotokea duniani. Ni sawa na kusema zamani tulikuwa na magari yanayotumia gia kuanzia moja hadi nne, lakini magari mengi hivi sasa ni automatiki," anasema.
Hata hivyo, Afande Sele anaamini watayarishaji wa muziki ni muhimu zaidi katika kutengeneza nyimbo za msanii au bendi kwa vile kazi yao huchukua takriban asilimia 20 au 30. Anasema mara nyingi kazi ya msanii ni kutunga na kuandika mashairi.
Msanii huyo mwenye maskani mjini Morogoro, anaamini muziki wa kizazi kipya utadumu kwa vile hata baadhi ya nyimbo zilizopigwa miaka saba hadi 10 iliyopita, kama vile wimbo wake wa Darubini Kali, Nikusaidieje wa Profesa Jay na Kamanda wa Daz Nunda bado zinapendwa.
"Wimbo kudumu kwa miaka mingi, inategemea ujumbe wake, upigaji wa ala na vionjo. Zipo nyimbo za baadhi ya bendi za zamani ukizisikiliza hivi sasa hazina mvuto kabisa," anasema.
Kiongozi wa B Band, Banana Zorro, ambaye ni mmoja wa wasanii nyota wa muziki wa kizazi kipya anasema aliamua kupiga muziki wa bendi baada ya kubaini kutegemea mauzo ya CD hakuwezi kumfikisha mbali.
"Faida ya muziki wa bendi ni kwamba, huwezi kutegemea mauzo ya CD. Unaweza kupata maonyesho sehemu mbalimbali ukaingiza fedha, lakini muziki ni muziki, uwe wa bendi au msanii mmoja, inategemea umejipanga vipi katika kuurekodi," anasema Banana.
Anasema wapo watayarishaji hodari katika kutengeneza muziki wa kizazi kipya, ambao wanaweza kumbadilisha msanii akaonekana mzuri na kwamba jambo la msingi ni kwa msanii kuwa mbunifu.
Akifafanua, Banana anasema mtayarishaji bora wa muziki anaweza kutambua kipaji cha msanii na kumwelekeza ni aina gani ya muziki inayomfaa na kumtayarishia nyimbo kulingana na aina hiyo ya muziki, hivyo kuwa utambulisho wake.
Barnaba Elias wa kundi la muziki la Tanzania House of Talent (THT), anasema kupiga muziki wa ala ni jambo muhimu katika kutafuta soko la muziki, lakini si kweli kwamba muziki wa kizazi kipya hauna mvuto.
“Hilo linategemea utunzi wa msanii na utengenezaji wa ala za muziki unaofanywa na mtayarishaji wa muziki," anasema msanii huyo.
Barnaba anasema binafsi aliamua kujifunza kupiga ala za muziki badala ya kutegemea muziki wa studio baada ya kusoma soko la muziki. Anasema muziki wa bendi ni mzuri na una mvuto zaidi ikilinganishwa na ule wa kompyuta.
"Muziki wowote ni mzuri, inategemea kazi yako. Wanaosema muziki wa kizazi kipya hauwezi kudumu wanakosea, ni kwa sababu tangu ulipoanza bado upo na umekuwa ukiipandisha chati Tanzania kimuziki," anasema.
Msanii Lucas Silas 'Dk. Leader' wa mkoani Tanga, anakiri muziki wa kizazi kipya umekusanya wasanii wengi wasio na vipaji, ambao baadhi wamepandikizwa au kujitosa kwenye fani kwa lengo la kupata umaarufu.
Akifafanua kauli yake, Dk. Leader anasema wasanii wasio na vipaji ni wale wasioweza kuimba kwa kufuata funguo za muziki, kwamba wapo ambao badala ya kuimba wanapayuka.
Ametaja aina nyingine ya wasanii wa aina hii kuwa ni wenye uwezo kifedha na wanalazimisha kuimba ili wapate umaarufu.
"Wengi wanatafuta pesa kwa sababu hawajui ala za muziki. Wakiimba ‘laivu’ inakuwa kichekesho. Teknolojia imerahisisha, lakini inatumaliza," anasema.
Msanii huyo anasema wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya wanashindwa kuimba wanapokuwa jukwaani (laivu) kutokana na kutokuwa na uzoefu huo na kwamba, muziki wa kompyuta umerahisisha kazi kwa sababu ni rahisi kwa msanii yeyote mwenye uwezo wa kuandika mashairi.
Msanii wa zamani wa kundi la Wagosi wa Kaya, John Evans 'Dk John' mwenye makazi mjini Tanga, anaamini muziki wa kizazi kipya umelenga biashara na ni wa kuiga kutoka kwa wasanii wa Marekani, ambao waliamua kutumia kompyuta ili kurahisisha kazi.
"Wasanii wengi hukimbilia kuandika mashairi na kuingia studio bila kuwa na ufahamu wowote kuhusu muziki. Tunapaswa kuwa wabunifu. Ndiyo sababu katika nyimbo zangu nimekuwa nikitumia zaidi ala za asili na kuimba kwa lafudhi ya Kidigo ili kuongeza mvuto," anasema.
Hata hivyo, Dk. John anasema wapo wanaoingia katika muziki kwa lengo la kujifunza na kuonyesha wanachokijua na kukipenda kwa mashabiki wa fani hiyo.
Licha ya kuwepo kwa kasoro hizo, Dk. John anaamini muziki huo utadumu kwa sababu ni biashara inayowaingizia baadhi yao mamilioni ya shilingi, ikiwa ni pamoja na malipo ya miito ya simu. Malipo hayo hufanywa na kampuni za simu kwa wasanii, ambao nyimbo zao hutumiwa na wateja kama miito ya simu.
Msanii nyota wa zamani wa kundi la East Coast, Pauline Zongo, anasema aliamua kuachana na muziki wa kizazi kipya na kujitosa kwenye dansi kwa lengo la kupima uwezo wake na kujiendeleza kimuziki.
Pauline anasema uamuzi wake wa kujiunga na bendi ya TOT Plus ulilenga kukuza kipaji chake cha muziki na pia kuwaonyesha mashabiki kwamba ana uwezo mkubwa katika fani hiyo.
"Huwezi kuwa mwanamuziki mzuri kama hujui kupiga ala yoyote ya muziki," anasema mwanamama huyo, ambaye ana uwezo wa kupiga gita, ngoma na kinanda.
Mwanamama huyo anasema hakujifunza muziki kutoka kwa mtu yeyote. Anasema kuna siku alilala akaota ndoto anapiga gita, ngoma, kinanda na kuimba.
Kwa mujibu wa Pauline, alipozinduka usingizini, aliamua kutimiza ndoto yake.
Pauline anasema awali, aliamua kujitosa katika muziki wa kizazi kipya baada ya kujitambua kwamba ana kipaji cha kuimba. Anakiri muziki huo unafanana na wa dansi, lakini unatofautiana katika uchezaji.
Muziki wa dansi huchezwa kwa kutingisha viungo vya mwili wakati wa kizazi kipya huchezwa kwa kuinyonganyonga mwili na wakati mwingine huongezewa nakshi kwa kuruka sarakasi.
Pauline anasema hivi sasa anaweza kupiga muziki wa miondoko tofauti, ikiwemo reggae, dansi na ragamuffin. Muziki wa reggae na ragamuffin huchezwa kwa kurukaruka.
"Kuna umuhimu kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kupiga ala za muziki, badala ya kutegemea muziki unaotengenezwa kwenye kompyuta," anasema mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT).
Pauline anasema ameamua kutoa ushauri huo ili wasanii wa fani hiyo wawe na uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, badala ya kutegemea kitu kimoja.
Anasema kubadilika kwa wasanii hakuwezi kuzifanya studio za kurekodi muziki zife au ajira hiyo kukoma.
Mtayarishaji wa muziki wa kizazi kipya, Ally Mohamed 'Baucha' anaamini gharama za kurekodi nyimbo studio kwa kutumia ala za muziki ndizo zinazowafanya wasanii wengi wakimbilie kurekodi nyimbo kwa kutumia kompyuta.
Gharama ya kurekodi wimbo kwa kutumia kompyuta inatofautiana kati ya watayarishaji, ambapo kiwango cha chini ni sh. 100,000, tofauti na kutumia ala, ambapo gharama ziko juu kwani wapiga ala pia huhitaji kulipwa, hivyo kuwa zaidi ya sh. 500,000.
"Tatizo pekee kwa sisi watayarishaji wa muziki ni ubunifu wa mipigo ya ala. Kama mtayarishaji wa muziki atatengeneza ala nzuri, muziki utadumu kwa muda mrefu. Si watayarishaji wote wamesoma au wana ujuzi huo," anasema.
Baucha anasema kazi kubwa ya mtayarishaji wa muziki ni kwenye kuchanganya mipigo ya ala za muziki na sauti kwa lengo la kuunogesha wimbo. Anasema kinyume cha hilo, kazi ya msanii haiwezi kuwa na mvuto.
No comments:
Post a Comment