KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 24, 2017

YANGA YAIPIGA NDANDA BAO 1-0, AZAM YAZIDI KUNG'ARA


YANGA SC imepata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
Shukrani kwake, mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji mpya kutoka kwa mahasimu, Simba SC, Ibrahim Hajib Migomba aliyefunga dakika ya 34 baada ya kazi nzuri ya beki wa kati, Kevin Patrick Yondan.
Beki wa kulia, Juma Abdul Mnyamani alimuanzishia kona fupi Yondan, ambaye alijitengeneza na kutia krosi maridadi iliyounganishwa nyavuni na Hajib kwa staili ya kujipinda maarufu kama baiskeli.

Lakini Yanga itamkosa kiungo wake mpya, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi katika mchezo wake ujao na Mtibwa Sugar Septemba 30, baada ya kuonyeshwa kadi ya njano na refa Jeonisya Rukyaa wa Kagera leo, ambayo inakuwa kadi yake ya tatu mfululizo.
Wakati huo huo, timu ya Azam FC, imeendelea kufanya kweli kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Lipuli bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam usiku wa Jumapili.
Kwa ushindi huo Azam FC imefanikiwa kuikamata Mtibwa Sugar baada ya kufikisha jumla ya pointi 10 zikiwa zinalingana kileleni huku ikiwa timu pekee ambayo haijaruhusu bao lolote tokea ligi hiyo ilipoanza Agosti 26, mwaka huu.
Bao pekee la Azam FC limefungwa na Mbaraka Yussuf dakika ya 11 akipokea pasi safi ya Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, likiwa ni bao lake la pili kwenye mechi ya pili mfululizo, lingine akiitungua timu yake ya zamani Kagera Sugar katika ushindi wa 1-0.
Nayo Mtibwa Sugar imepunguzwa kasi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment