KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 8, 2017

SIMBA, AZAM KUONYESHANA UBABE LEO, PAMBANO KUANZA SAA 10 JIONI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefanya mabadiliko kidogo ya muda wa kuanza mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Azam FC na Simba SC.
 
Mchezo huo utafanyika kesho Jumamosi Septemba 9, 2017 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salam kama ulivyopangwa awali.


Kuhusu muda, mchezo huo ulipangwa ufanyike kuanzia saa 1.00 usiku, lakini sasa utaanza saa 10.00 jioni - uamuzi uliofanyika baada ya kupokea ushauri kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda.


Mbali ya mchezo huo, mechi nyingine ya kesho Jumamosi Septemba 9, mwaka huu  itakuwa ni kati ya Tanzania Prisons na Majimaji ya Songea uliopangwa kufanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.


Mechi nyingine za Ligi Kuu ya Vodacom, zitakuwa Jumapili Septemba 10, mwaka huu ambako Njombe Mji FC na Young Africans SC zitacheza Uwanja wa Sabasaba mjini Makambako wakati Mtibwa Sugar FC na Mwadui FC ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.


Kadhalika Lipuli FC itacheza na Stand United FC Uwanja wa Samora mjini Iringa wakati Singida United itacheza na Mbao kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.


Pia Kagera Sugar itacheza na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba huku Mbaya City ikiwa wenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linapenda kuwatangazia wananchi kuwa viingilio katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Azam na Simba.

Viingilio vitakuwa shilingi elfu kumi (Sh 10,000) kwa Jukwaa Kuu ambalo lina uwezo wa kubeba mashabiki 1,000 tu walioketi, wakati mzunguko (popular) kiingilio kitakuwa ni shilingi elfu saba tu (Sh 7,000).

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linapenda kuwatangazia wanafamilia ya mpira wa miguu kukata tiketi kuanzia leo Jumatano Septemba 6, mwaka huu ili kujiepusha na usumbufu wa aina yoyote.

Kadhalika tunapenda kuwatangazia wananchi kwamba kwa ye yote ambaye hana tiketi ni vema wasiende uwanjani kwani ujio wake hautakuwa na tafasiri nyingine zaidi ya kuonekana kuwa ni mleta fujo.

Vyombo vya usalama vitakuwa makini kudhibniti kila aina ya vurugu uwanjani hapo hasa ikizingatiwa kuwa mchezo huo utafanyika wakati jua limezama.

No comments:

Post a Comment