KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 30, 2014

ALLY BAUCHA AJA NA CHAMPODODORAGE ATAKA SHERIA YA BMT IREKEBISHWE, AITAKA Z'BAR ISAHAU UANACHAMA WA FIFA, NKAMIA AMUONYA MALINZI KUBADILI JINA LA STARS


MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ameikosoa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kutaka ifanyiwe marekebisho ili iendane na mabadiliko ya ulimwengu wa michezo.


Akichangia Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliyowasilishwa Bungeni mjini Dodoma jana asubuhi, Rage alisema Sheria ya BMT imepitwa na wakati kwa sababu ina vitu vingi ambavyo vinavyozungumzia enzi za ujima ambazo kwa sasa havipo.

"Ipo Sheria ya BMT ya mwaka 1967 ambayo kwa mara ya mwisho ilifanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 1971. Vitu vingi vilivyomo kwenye Sheria hiyo vimepitwa na wakati. Mfano, inazungumzia kuwania uongozi lazima uwe mwanachama wa TANU, chama ambacho kwa sasa hakipo," amesema Rage.

Aidha, Rage ametumiwa fursa hiyo kuwaomba wanachama na wapenzi wa Simba watulie kipindi hiki ambacho klabu hiyo iko katika mchakato wa uchaguzi mkuu.

"Ninawaomba wanachama wa Simba watulie katika kipindi hiki cha kusaka viongozi wapya ili masuala yote yanayohusu mchakato wa uchaguzi mkuu yashughulikiwe kwa misingi na taratibu zilizopo za mpira wa miguu," amesema Rage.

Katika hatua nyingine, Rage, ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini (CCM) amelitaka BMT kuhakikisha linakuwa na kipengele katika Katiba yake inayokataza watu wanaopeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia.

"Ukiangalia Katiba za TFF, CAF na FIFA zinakataza masuala ya soka kuingiliwa na serikali na kupelekwa katika mahakama za kiraia. BMT iwe na kifungu cha sheria kinachokataza watu wanaopeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia ili iende sanjari na Katiba za mashirikisho hayo," amesema Rage.

Rage, ambaye anamaliza muda wake wa miaka minne wa kuiongoza Simba Juni 29, mwaka huu tangu aingie rasmi madarakani Mei 10, 2010, amewataka Wazanzibar kutopoteza muda wa kusaka uanachama FIFA kwa vile suala hilo ni sawa na ndoto za mchana.

"Wanachama wote wa FIFA, isipokuwa zile nchi maalum kisoka za Scoatland na Wales, ni wanachama wa UN (Umoja wa Mataifa). Zanzibar si mwanachama wa UN, hivyo hawezi kuwa mwanachama wa FIFA. Nimeamua kulisema hili mapema ili Waziri asisumbuke kuulizwa maswali juu ya hatua iliyofikiwa ya Zanzibar kusaka uanachama katika shirikisho hilo la soka la kimataifa," amesema zaidi Rage.

Wakati huo huo, serikali imelitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuachana na mpango wa kubadilisha jina la timu ya taifa (Taifa Stars) badala yake ijikite katika kuboresha kikosi cha timu hiyo.

Akijibu maswali ya wabunge leo asubuhi Bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia (pichani chini), amesema hakuna haja ya kubadili jina hilo kwa kuwa kufanya hivyo serikali haioni kama kutakuwa na mantiki.
"Tumepokea maoni ya TFF kutaka kubadili jezi za timu ya taifa kwa kuwa rangi ya bluu kwenye TV inaleta matatizo. Pia wamependekeza kubadili jina la timu ya taifa. Serikali inaona hakuna haja ya kubadili jina badala yake wajikite katika kubadili mchezo wenyewe," amesema Nkamia.

Mapema mwezi huu, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema jijini Dar es Salaam kuwa watakusanya maoni ya Watanzania kupata jina jipya la timu ya taifa na aina ya jezi ambazo timu hiyo itakuwa inavaa.

SAMATTA, ULIMWENGU KUIONGEZEA NGUVU STARSKlabu ya TP Mazembe imewaruhusu wachezaji wake Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kujiunga na timu ya Taifa (Taifa Stars) ambayo tayari imewasili Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika.

Taifa Stars itacheza na Zimbabwe (Mighty Warriors) katika mechi ya marudiano raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Mechi hiyo itachezwa Jumapili (Juni 1 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare.

Samata na Ulimwengu watawasili Harare kesho (Mei 30 mwaka huu) saa 3.40 usiku kwa ndege ya Kenya Airways. Watajiunga na TP Mazembe mara baada ya mchezo huo ambapo Juni 2 mwaka huu watakwenda moja kwa moja Ndola, Zambia ambapo timu yao imepiga kambi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

U15 TANZANIA YASHIKA NAFASI YA PILI AYG
Tanzania imeshika nafasi ya pili kwenye Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya jana (Mei 29 mwaka huu) kuilaza Afrika Kusini mabao 2-0.

Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa SSKB jijini Gaborone ambapo kwa matokeo hayo Tanzania imetwaa medali ya fedha baada ya kushika nafasi ya pili. Nigeria ndiyo ilishika nafasi ya kwanza na kutwaa medali ya dhahabu.

Tanzania imemaliza ikiwa na pointi kumi ambapo ilishinda mechi tatu, sare moja na kupoteza moja mbele ya Nigeria.

Katika mechi ya kwanza ilitoka sare ya bao 1-1, ikawafunga Botswana 2-0, Swaziland wakachapwa 3-0 na baadaye kuwafunga Afrika Kusini 2-0. Timu ya Tanzania inayofundishwa na kocha Abel Mtweve ilifungwa na Nigeria mabao 2-0.

Wachezaji 16 waliounda kikosi hicho cha Tanzania katika michezo hiyo inayomalizika leo (Mei 30 mwaka huu) ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.

Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland wakati Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) zilijitoa dakika za mwisho.

Thursday, May 29, 2014

MWAMBUSI KOCHA BORA LIGI KUU, TAMBWE MFUNGAJI BORA, SHARRIF KIPA BORA, KIPRE TCHETCHE MWANASOKA BORA


Kocha Mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi ameshinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa 2013/2014.

Hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali ilifanyika jana (Mei 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mbali ya tuzo hiyo, Kocha Mwambusi ambaye hivi sasa yuko nchini Sudan na timu yake kwenye michuano ya Nile Basin alipata pia zawadi ya kitita cha sh. milioni 7.8.

Aliyeshinda tuzo ya kipa bora ni Hussein Shariff wa Mtibwa Sugar aliyepata sh. milioni 5.2 wakati Amisi Tambwe wa Simba aliibuka na tuzo ya mfungaji bora. Tambwe naye alipata sh. milioni 5.2.

Mchezaji bora wa VPL kwa msimu wa 2013/2014 ni Kipre Tchetche wa Azam FC aliyejipatia sh. milioni 5.2. Tuzo ya refa bora imetwaliwa na Israel Mujuni aliyezawadiwa sh. milioni 7.8.

Yanga iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi na kupata sh. milioni 37, pia ilipata sh. milioni 16 baada ya kushinda tuzo ya timu yenye nidhamu ya hali ya juu. Sh. milioni 21 za mshindi wa nne zilikwenda kwa timu ya Simba.

Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC walipata sh. milioni 75 wakati Mbeya City ilipata sh. milioni 26 kwa kushika nafasi ya tatu.

RAIS MALINZI ATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA KOCHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso Mwale.

Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha Mwale, na kuongeza kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano wa kuigwa kwa makocha wazalendo waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.

Rais Malinzi amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mwale, na kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwao.

Mwale (51) alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha katika barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini kujiunga na timu yake kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory Coast.

TAIFA STARS KWENDA ZIMBABWE LEO


Msafara wa watu 30 wa Taifa Stars unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi unaondoka kesho alfajiri (Mei 29 mwaka huu) kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.
Mechi hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua jijini humo saa 5 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.
Msafara wa Taifa Stars ambayo ambayo jana (Mei 27 mwaka huu) ilicheza mechi ya kujipima nguvu na Malawi na kushinda bao 1-0, na utarejea nchini Juni 2 mwaka huu unaongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Wakati huo huo, mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.
Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08, gharama za kuchapa tiketi sh. 225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24, gharama za mechi sh. 1,375,218.98 na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 4,469,461.69.

MBEYA CITY YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA NILE BASIN
MBEYA City imetinga Robo Fainali za michuano ya Nile Basin inayoendelea nchini Sudan kufuatia sare ya bila kufungana na Enticelles ya Rwanda usiku huu Uwanja wa Khartoum.

Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City imalize na pointi nne baada ya mechi tatu, ikiwa katika nafasi ya pili nyuma ya AFC Leopards ya Kenya walioongoza kundi kwa pointi zao tisa. 
Enticelles imemaliza nafasi ya pili kwa pointi zake mbili na Academie Tchite ya Burudi imemaliza mkiani mwa Kundi B kwa pointi moja iliyovuna kwenye sare na timu ya Rwanda.

Katika mchezo mwingine wa leo wa kundi hilo michuano hiyo inayoshirikisha mabingwa wa Kombe la FA au washindi wa pili wa Ligi Kuu za nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leopard imeifunga Tchite 1-0.

Bao pekee la Ingwe limefungwa na kiungo wa zamani wa Simba SC ya Tanzania, Mganda Mussa Mudde, ambalo hilo linakuwa bao lake la pili kwenye michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu, baada ya awali kuwafunga Mbeya City, Leopards ikishinda 2-1.

Mbeya City na AFC Leopards sasa zinasubiri kujua wapinzani wao katika Robo Faibali baada ya mechi za mwisho kesho usiku.

Mbeya City; David Burhan, Yussuf Abdallah, Hamadi Kibopile, Christian Sembuli, Yohanna Morris, Athony Matogolo, Deus Kaseke, Steven Mazanda, Paul Nonga, Mwagane Yeya na Themi Felix.

Enticelles; Nsanganira Djuma, Ndayisenga Mbanyi, Hategekimana Abdallah, Nkusi Prince, Nahimana Isiyaka, Gasangwa Salum, Ndikumasabo Ibrahim, Ismail Mugabo, Manishimwe Yves, Arafat Bahame na Herorimana Bosco.

Wednesday, May 28, 2014

TAIFA STARS YAICHAPA MALAWI 1-0


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana iliichapa Malawi bao 1-0katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taifa Stars iliuanza mchezo huo kwa kasi na kufanya shambulizi la nguvu kwenye lango la Malawi dakika ya tano, lakini shuti la Simon Msuva lilitoka nje ya lango.

Dakika ya 17, Kevin Friday alipewa pasi akiwa nje kidogo ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilipaa juu.

Bao la Taifa Stars lilifungwa na Amri Kiemba dakika ya 37 baada ya kuunganisha pasi maridhawa kutoka kwa Shomari Kapombe. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Malawi ilifanya mashambulizi ya nguvu kwenye lango la Taifa Stars dakika ya 46, 63 na 80, lakini mara zote mashuti ya Rodrick Gonani yalitoka nje.

RECHO WA BONGO MOVIE AFARIKI


MSANII nyota wa filamu nchini, Rachel Haule 'Recho', amefariki dunia.

Recho alifariki dunia juzi katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bongo Movie, Steve Nyerere, alisema jana kuwa, Recho alipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua.

Kwa mujibu wa Nyerere, msanii huyo alijifungua kwa njia ya upasuaji, lakini mtoto wake alifariki muda mfupi baadaye wakati hali ya msanii huyo ikiwa mbaya.

Alisema baada ya msanii huyo kuwa mahututi, alihamishiwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu, lakini hali ilikuwambaya zaidi na kufariki dunia.

Alisema kifo cha msanii huyo ni pigo kubwa katika tasnia ya filamu nchini kwa vile kifo chake kimetokea siku chache baada ya kufariki kwa Adam Kuambiana.

"Hili ni pigo kubwa sana kwetu, lakini hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kuwa yeye ndiye mwamuzi wa kila jambo. Tunachopaswa kufanya ni kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu,"alisema.

Recho alianza uigizaji mwaka 2009, akicheza maigizo katika kikundi cha Mburahati kabla ya kuanza kucheza filamu.

Alizaliwa mkoani Ruvuma katika wilaya ya Songea na kupata elimu ya msingi katika shule ya Luida iliyoko wilayani humo.

Miaka michache baadaye, alihamia Dar es Salaam na kujiunga na shule ya sekondari ya Baptist iliyoko Magomeni kabla ya kuhamia sekondari ya Hanga.
Baada ya kumaliza sekondari, alijiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma cha Magogoni.

MBEYA CITY YAPIGWA 2-1 NA AFC LEOPARDSNa Mwandishi Wetu

MBEYA City imefungwa mabao 2-1 AFC Leopard ya Kenya katika mchezo wa Kundi B michuano ya Nile Basin uliofanyika kwenye Uwanja Khartoum, Sudan.


Mabao yaliyozamisha Mbeya City katika mchezo wa mashindano hayo mapya ya Baraza la Soka la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inayofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu yamefungwa na kiungo wa zamani wa Simba SC Mganda Mussa Mudde na Mkenya Paul Were.

Bao la Mbeya City limefungwa na kiungo Deus Kaseke na sasa Leopard inaendelea kuishi kileleni mwa Kundi B kwa kufikisha pointi sita, wakati Mbeya City yenye pointi tatu inabaki nafasi ya pili.

Mchezo huo wa michuano inayoshirikisha mabingwa wa Kombe la FA na washindi wa pili wa Ligi Kuu za nchi wanachama wa CECAFA, ulichezeshwa na refa Khalil Walida aliyesaidiwa na Mohammed Abdallah wote wa Sudan na Bogoreh Farhan wa Djibouti.

Mbeya City; David Burhan, Mwagane Yeya, Hamad Kibopile, Deo Julius, Yohanna Morris, Antohny Matogolo, Deus Kaseke, Steven Mazanda, Paul Nonga, John Kabanda na Themis Felix.

AFC Leopard; Patrick Matasi, Paul Were, Edwin Wafula, Eric Masika, Joseph Shikokoti, Mussa Mudde, Austin Ikenne, Juma Abdallah, Jackson Saleh, Benard Mangoli na Noah Wafula.

Monday, May 26, 2014

MISS DAR CITY CENTRE APATIKANA


Hatimaye mbio za kumsaka Miss Dar City Centre 2014 zimehitimishwa juzi katika ukumbi wa Dar es Salaam Free Market baada ya mshiriki namba kumi na saba,  Jihan Dimechk kutawazwa mshindi wa Miss Dar City centre 2104. Picha na Justine Kazaura wa Light Photo Studio
KIINGILIO TAIFA STARS VS MALAWI BUKU TANOKiingilio cha chini cha mechi ya kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (Flames) itakayofanyika Jumanne (Mei 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.

Washabiki watakaolipa kiingilio hicho ni kwa wale watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.

Mechi hiyo itaanza saa 11 kamili jioni ili kutoa fursa kwa washabiki wengi zaidi kuishuhudia kwa vile itakuwa ni siku ya kazi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili asubuhi ya siku hiyo hiyo ya mechi kutoka Tukuyu mkoani Mbeya ambapo imepiga kambi yake chini ya Kocha Mholanzi Mart Nooij.

Malawi (Flames) inayonolewa na mchezaji wake wa zamani Young Chidmozi tayari ipo nchini kwa ajili ya mechi hiyo inayotumiwa na timu zote kama maandalizi ya mwisho kwa ajili mechi za mchujo za Kombe la Afrika (AFCON).

Wakati Stars kwenye mechi za AFCON itarudiana na Zimbabwe jijini Harare, Flames nayo itakuwa ugenini N’djamena kukabili Chad.

Sunday, May 25, 2014

MAMIA WAMZIKA AMINA NGALUMA
MWIMBAJI nyota wa zamani wa bendi za muziki wa dansi za African Revolution na Double M Sound, Amina Ngaluma amezikwa.

Mazishi ya mwanamuziki huyo yalifanyika jana katika makaburi ya Machimbo Mnarani, Kitunda, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Amina alifariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand baada ya kuugua kwa muda mfupi na mwili wake ulirejeshwa nchini Ijumaa iliyopita kwa ndege.

Mwanamuziki huyo alikuwepo Thailand kwa zaidi ya miaka miwili, akipiga muziki katika bendi ya Jambo Survivors.

Baadhi ya wanamuziki wakongwe na chipukizi ni miongoni mwa mamia ya watu waliojitokeza kumsindikiza mwanadada huyo katika safari yake ya mwisho duniani.

Miongoni mwa wanamuziki wakongwe waliohudhuria mazishi hayo ni John Kitime, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Ally Choki, Muumin Mwinjuma, Abdalla Mgonahazelu, Rogert Hegga na Super Nyamwela.

Wakizungumza na blogu hii wakati wa mazishi hayo, baadhi ya wanamuziki walikielezea kifo cha Amina kuwa ni pigo kubwa katika tasnia hiyo kutokana na uhodari wake wa kutunga na kuimba nyimbo zenye mvuto.

MBEYA CITY YAANZA VIZURI KOMBE LA NILE BASINWAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano mipya ya klabu ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iitwayo Nile Basin, Mbeya City wameanza vizuri leo baada ya kuifunga mabao 3-2 Academie Tchite ya Burundi mjini Khartoum, Sudan.


Mabao ya Mbeya City katika mchezo huo wa Kundi B yamefungwa na Paul Nonga dakika ya 15, mshambuliaji mpya Themi Felix kutoka Kagera Sugar dakika ya 27 na Mwagane Yeya dakika ya 37. Mabao ya timu ya Burundi yamefungwa na Rashid Patient dakika ya 10 na Munirakiza Cedric dakika ya 68.

Ushindi huo unawaweka Mbeya City katika nafasi nzuri ya kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo.

Mapema katika mechi za ufunguzi jana, mabao saba yalitinga nyavuni, Victoria University ya Uganda ikiilaza 1-0 Malakia ya Sudan Kusini, El-Merreikh waliichapa 3-0 Polisi ya Zanzibar na El-Shandi waliilaza 2-1 Dkhill ya Djibouti.

Michuano hiyo inashirikisha mabingwa wa Kombe la FA na washindi wa pili wa Ligi Kuu wa nchi wanachama wa CECAFA. Mbeya City imechukua nafasi ya Azam FC, washindi wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, ambao wamejitoa.

Simba SC ambao wangechukua nafasi ya Azam, wakati taarifa inakuja ya kufanyika kwa mara ya kwanza michuano hiyo, walikuwa wamekwishavunja kambi na wachezaji wao wote walikuwa wameruhusiwa likizo.

TAIFA STARS KUVAANA NA MALAWI JUMANNE
Taifa Stars na Malawi (Flames) zinapambana Jumanne (Mei 27 mwaka huu) katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni.

Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Taifa Stars kujipima kabla ya kucheza mchezo wa marudiano wa michuano ya Afrika na Zimbabwe (Mighty Warriors) utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu jijini Harare.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya chini ya Kocha wake Mart Nooij kujiandaa kwa mechi dhidi ya Malawi na ile ya Zimbabwe.

Malawi imewasili leo mchana (Mei 24 mwaka huu) kwa ndege ya Malawian Airlines kwa ajili ya mchezo huo ikiwa na msafara wa watu 27, na imefikia kwenye hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi jijini Dar es Salaam.

Flames inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Young Chidmozi inatarajia kufanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Baada ya mechi hiyo, Malawi itakwenda moja kwa moja nchini Chad kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika itakayochezwa Mei 30 mwaka huu jijini Ndjamena.

FAINALI BEACH SOCCER KUCHEZWA JUMAPILI
Fainali ya michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (beach soccer) kati ya timu za Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) inachezwa kesho (Mei 25 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa wikiendi iliyopita.

Mgeni rasmi katika fainali hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam Tv atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na itaanza saa 4.15 asubuhi. Fainali hiyo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA kuanzia saa 3 kamili asubuhi.

Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni.

Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ).

Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.

Wednesday, May 21, 2014

NGORONGORO HEROES YAENDA NIGERIA


Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) chenye watu 25 kinaondoka kesho alfajiri kwenda Nigeria kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).

Mechi hiyo itachezwa Jumamosi (Mei 24 mwaka huu) katika Jiji la Kaduna kwenye Jimbo la Kaduna ambalo lipo katikati ya Nigeria. Msafara wa timu hiyo unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi unaondoka kwa ndege ya Ethiopian Airlines.

Ngorongoro Heroes inayonolewa na Kocha John Simkoko ilipoteza mechi ya kwanza iliyofanyika nyumbani jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0.

Mwamuzi Alhadi Allaou Mahamat wa Tchad ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Atasaidiwa na Issa Yaya, Alfred Madjihoudel na Idriss Biani wote kutoka Tchad. Kamishna ni Aboubakar Alim Konate wa Cameroon.

TIMU YA U15 YAWASILI GABORONE
Timu ya Tanzania ya umri chini ya miaka 15 imewasili salama jijini Gaborone, Botswana kwa ajili ya michezo ya Afrika ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Mei 22 mwaka huu dhidi ya Mali.

Kikosi hicho cha wachezaji 16 chini ya Kocha Abel Mtweve kimetua jijini Gaborone jana (Mei 19 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South African Airways. Michezo hiyo itamalizika Mei 30 mwaka huu.

Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Tanzania ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.

Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland.

Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambazo nazo zilikuwa zishiriki kwenye michezo hiyo zimejitoa dakika za mwisho.

USAJILI WA WACHEZAJI KUANZA JUNI 15Usajili wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2014/2015) unaanza Juni 15 hadi
Agosti 3 mwaka huu wakati kipindi cha kutangaza wachezaji walioachwa au kusitishiwa
mikataba ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu.

Kipindi cha kwanza cha uhamisho wa wachezaji ni kuanzia Juni 15 mwaka huu hadi Julai
30 mwaka huu. Kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Agosti 4 na 11 mwaka
huu. Kuthibitisha usajili hatua ya awali ni Agosti 12 hadi 14 mwaka huu.

Usajili hatua ya pili utakuwa kati ya Agosti 14 na 29 mwaka huu. Kupitia na kutangaza
majina ya pingamizi hatua ya pili ya usajili ni kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4 mwaka
huu. Uthibitisho wa usajili hatua ya pili ni Septemba 5 na 6 mwaka huu.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu,
na ratiba inatarajiwa kutoka mwezi mmoja kabla (Julai 24 mwaka huu).

TAIFA STARS, ZIMBABWE ZAINGIZA MILIONI 63
Mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe iliyochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 63,345,000.

Mapato hayo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 yametokana na washabiki 11,079 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000.

Mgawo wa mapato hayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 9,662,796.61, gharama za kuchapa tiketi sh. 6,000,000, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 7,152,330.51, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 9,536,440.68 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa pamoja wamepata sh. 30,993,432.20.

WASHABIKI KWENDA HARARE KUSHANGILIA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaandaa utaratibu utakaowawezesha washabiki kwenda jijini Harare, Zimbabwe kushuhudia mechi ya Taifa Stars.

Mechi hiyo ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa ajili ya fainali zitakazochezwa Morocco mwakani itafanyika Jumapili (Juni 1 mwaka huu) jijini Harare.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Usafiri huo utakuwa wa basi ambapo washabiki wanatarajiwa kuondoka siku ya Ijumaa na kuwasili Jumapili mchana jijini Harare ambapo watashuhudia mechi na kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo.

Washabiki wanatakiwa kuwa na hati za kusafiria (pasipoti), nauli ya kwenda na kurudi itakuwa sh. 300,000.

Tuesday, May 20, 2014

MWILI WA KUAMBIANA ULIVYOAGWA LEO LEADERS CLUB, KINONDONI, DAR ES SALAAM


Hivi ndivyo mamia ya wasanii wa filamu nchini walivyojitokeza kuuaga mwili wa mwigizaji mwenzao, marehemu Adam Kuambiana, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita. Mwili wa Kuambiana uliagwa kwenye viwanja vya Leaders, vilivyoko Kinondoni, Dar es Salaam. Serikali iliwakilishwa na Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Dk. Fenella Mukangara. (Picha zote kwa hisani ya blogu ya Michuzi).

MWILI WA AMINA NGALUMA KUREJESHWA DAR IJUMAAMWILI wa mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand, Amina Ngaluma ‘Japanese’ unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Ijumaa wiki hii.

Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Rashid Sumuni tayari taratibu muhimu kuhusiana na kuuleta mwili huo nyumbani zimefanyika na wana amini mambo yataenda kama wanavyotarajia.

“Naomba niwajulishe kuwa mwili wa mke wangu utaondoka Thailand Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na utawasili Dar es Salaam siku inayofuata saa tatu usiku.

“Tunaamini kama mambo yataenda kama tulivyopanga baada ya mwili kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi mwenzetu. Msiba upo kwa wazazi wa marehemu Kitunda, Machimbo, Dar es Salaam ambako ndiko maziko yatafanyika.

“Kimsingi imekuwa ngumu kusema tutazika lini, kwa sababu bado mwili haujaletwa, lakini tayari familia kwa kushirikiana na sehemu alikokuwa anafanya kazi na Watanzania wengine waishio kule tumeshamaliza taratibu zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta mwili nchini,” alisema Sumuni kwa masikitiko.

Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuwa karibu na familia yao wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini akiomba wanapotaka kutoa habari kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika wa familia ili kupata taarifa sahihi zaidi.

Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Alhamisi iliyopita kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor.

Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’, Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.

Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.

Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.

Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.

Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili, Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’.

Shiwata yawalilia Amina na Kuambiana
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA)umepokea kwa majonzi kifo cha mwanamuziki mashuhuri na maarufu wa mwanamuziki wa dansi nchini,Amina Ngaluma "Japanese" aliyefariki nchini Thailand.

Marehemu Ngaluma aliyekuwa mwanachama wa SHIWATA atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoyafanya akiwa mwanamuziki wa kike mwenye kipaji cha kutunga,kuimba na kutawala jukwaa katika maonesho ya akiwa na bendi mbalimbali ikiwemo Tam Tam, Double M,Tanzania One Theatre (TOT).

Ngaluma pia amewahi kufanya maonesho katika bendi za nje ya nchi kama Kenya na Thailand ambako amepatwa na mauti akiwa akifanya maonesho katika moja ya hoteli za kitalii.

SHIWATA inachukua nafasi hii kutoa pole familia ya Mzee Ngaluma kwa kuondokewa na mtoto wao mpendwa ambaye mbali ya mchango wake ulisaidia familia yake lakini pia taifa limepata pengo kwani alitumia kipaji chake cha sanaa kuelimisha, kuburudisha na kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi.

Mtandao pia unaungana na familia ya msanii wa Bongo Movie, Adam Kuambiana katika msiba uliomkuta juzi wakati mchango wake bado unahitajika katika fani hiyo.

Mchango wa Kuambiana umeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu nchini Tanzania kwa uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kuigiza na kuongoza filamu alizowahi kucheza kama ya Salt.

Sunday, May 18, 2014

TAIFA STARS YAIPIGA ZIMBABWE 1-0


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana iliwatoa kimasomaso Watanzania baada ya kuilaza Zimbabwe bao 1-0 katika mchezo wa awali wa michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika uliofanyika katika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kutokana na ushindi huo, Taifa Stars sasa inahitaji sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo mjini Harare.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi kwa kila timu kushambulia lango la mwenzake ambapo katika dakika ya tatu, Stars walikosa bao wakati John Bocco alipounganisha kwa kichwa krosi ya Thomas Ulimwengu, lakini mpira ulidakwa na kipa George Chigova wa Zimbabwe.

Zimbabwe nayo ilijibu mashambulizi ambapo katika dakika ya 11, shuti lililopigwa na Mahachi lilidakwa na kipa Munishi wa Stars.

Stars iliendeleza mashambulizi katika lango la Zimbabwe na katika dakika ya 13, Bocco aliandika bao pekee na la ushindi baada ya kumalizia vyema pasi iliyopigwa na Ulimwengu.

Baada ya bao hilo, kila timu iliongeza kasi ya mashambulizi huku Zimbabwe ikihaha kusawazisha bao hilo.

Mashambulizi hayo yaliendelea kwa kila upande kushambulia lango la mwenzake na hadi mapumziko, Stars ilikuwa ikiongoza kwa bao hilo moja dhidi ya Zimbabwe.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikishambulia ngome ya mwenzake. Hata hivyo, Zimbabwe ilitawala mchezo huku ikitafuta bao kwa nguvu zote, lakini hadi kipenga cha mwisho, Stars ilimudu kulilinda goli lake.

Stars: Deogratius Munishi,Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.

Zimbabwe: George Chigova, Partson Jaure ,Danny Phiri, Hardlife Zvirekwi, Stephen Alimwenda, Tendai Ndoro, Milton Nkube,Kudakwashe Manachi, Curthbert Malajila Peter Moyo na Eric Chipeta.

MWILI WA AMINA NGALUMA KUREJESHWA NCHINI KWA MAZIKO

 
MWILI wa mwanamuziki Amina Ngaluma 'Japanese Girl' aliyefariki dunia nchini Thailand wiki iliyopita, huenda ukarejeshwa nchini kwa ajili ya kufanyiwa maziko wiki ijayo.

Amina ni mwanamuziki wa zamani wa bendi za African Revolution 'Tamtam' na Double M Sound, zilizokuwa zikiongozwa na Muumin Mwinjuma.

Hadi mauti yalipomkumba, Amina alikuwa akiimbia bendi ya Jambo Survivors iliyokuwa na mkataba wa miaka minne nchini Thailand, akiwa na akina Ramadhani Kinguti na Hassan Show.

Habari za uhakika kutoka Thailand zimeeleza kuwa, Amina alifariki akiwa hospitali, ambako alilazwa kwa ajili ya kufanyiwa operesheni ya kichwa.

Mume wa marehemu, Rashid Sumuni, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshaanza kufanya maandalizi ya kuurejesha mwili wa marehemu nchini.

"Tunasubiri taratibu za kuurejesha mwili kutoka Thailand. Kwa sasa tunafanya mipango ya kutafuta nyaraka kutoka ubalozi wa Tanzania nchini Singapore kwa vile hatuna ubalozi Thailand,"alisema Sumuni.

Sumuni, ambaye ni mmoja wa wapiga gita hodari la solo nchini, alisema awali alipata taarifa kutoka kwa kiongozi wa Jambo Survivors kuhusu kuugua kwa mkewe na kwamba walimpeleka hospitali kupatiwa matibabu.

Aliongeza kuwa, alizungumza na Amina kwa mara ya mwisho Alhamisi iliyopita na kumuahidi kwamba angempigia simu Jumamosi kumpa maelekezo fulani, ambayo hakuweza kuyajua.

Sumuni alidokeza pia kuwa, katika mazungumzo hayo, Amina alimwelezea kuhusu hali ya kutokuelewana iliyojitokeza kati yake na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo.

"Aliniambia kuna mambo walikuwa hawaelewani lakini nilimpa moyo na kumtaka afanyekazi,"alisema.

Kwa mujibu wa Sumuni, yeye na mkewe walipanga kuendeleza maisha yao hapa nchini baada ya Amina kumaliza mkataba wake na bendi ya Jambo.

Licha ya kuishi mbali na mkewe, Sumuni alisema walikuwa wakipendana na kuheshimiana.

MWANAMUZIKI AMINA NGALUMA 'JAPANESE GIRL' AFARIKI THAILANDAliyewahi kuwa mwanamuziki wa dansi wa bendi za African Revolution 'Wana tam tam' na Double M, enzi hizo chini ya uongozi wa Muumin Mwinjuma, Amina Ngalum A.K.A Japanese (pichani enzi za uhai wake) amefariki dunia nchini Thailand, ambako alikuwa akifanya shughuli zake za kimuziki.

Akizungumza na mtandao huu, mtoaji wa habari hizi, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wake katika bendi ya Tam Tam, Asha Baraka, amesema kuwa Amina amefariki dunia wakati akifanyiwa upasuaji.

''Imeelezwa kuwa Amina alianza kuugua ghafla, huku akilalamika kuwa kichwa kinamuuna na tumbo, na ndipo alipokwenda hospitali kwa ajili ya kupima na kuambiwa kuwa alikuwa na uvimbe kichwani na hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji,"alisema.

Aidha ilielezwa kuwa uvimbe huo ulikuwa ukitoa damu na baada ya kuanza kufanyiwa upasuaji hakuweza kuamka tena na ndipo umauti ulipomfika'.

Mpaka mauti yanamfika, Amina alikuwa mwanamuziki wa bendi ya Jambo Survivors. Msiba upo Kipunguni B, Machimbo jijini Dar es Salaam.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU AMINA MAHALI PEMA. AMEN.

STARS, ZIMBABWE USO KWA USO LEOKocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo anawafahamu wachezaji wengi.

Amesema wachezaji wanaounda kikosi chake ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.

Nooij amesema ujio wa washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.

Samata na Ulimwengu watawasili nchini Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.

Wachezaji waliopo kambini kwa sasa ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin Friday.

Wakati huo huo, timu ya Zimbabwe (Mighty Warriors) inawasili kesho alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 27. Kesho saa 4 asubuhi (Mei 17 mwaka huu) Kocha wa timu hiyo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zinaanza kuuzwa kesho (Mei 17 mwaka huu) kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, OilCom Ubungo, Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala. Viingilio ni sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 tu.

MDAU AAHIDI WACHEZAJI MIL 5/-
Mdau mmoja wa mpira wa miguu ambaye hataki jina lake litajwe ameahidi kutoa sh. milioni tano kwa wachezaji wa Taifa Stars iwapo wataifunga Zimbabwe katika mechi ya Jumapili.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linamshukuru mdau huyo, na linatoa mwito kwa wadau wengine wajitokeze kutoa motisha kwa Taifa Stars.

Bonasi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa wachezaji wa Taifa Stars itatolewa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

TFF YAOMBOLEZA VIFO VYA WASHABIKI DR CONGO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- FECOFA, Omar Constant kutokana na vifo vya washabiki.

Washabiki 12 walipoteza maisha uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya nchi hiyo kati ya TP Mazembe na AS Vita iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tata Raphael, jijini Kinshasa.

“Tumeguswa na msiba huo mzito, tunatoa salamu za rambirambi kwako (Rais wa FECOFA), familia za marehemu pamoja na wadau wote wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,” imesema sehemu ya barua hiyo ya Rais Malinzi.

KOZI ZA UKOCHA LESENI A, B KUFANYIKA JUNI
Kocha a ukocha wa mpira wa miguu kwa ajili ya leseni A na B zinazotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) zitafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 2 mwaka huu.

Ada kwa kozi zote ni sh. 300,000 ambapo wale watakaofanya ya A (equivalent) itaanza Julai 21-26 mwaka huu. Washiriki wa kozi hiyo ni wale wenye leseni B za ukocha za CAF.

Kwa wale watakaoshiriki kozi ya leseni B ambao ni wale wenye leseni C watakuwa na vipindi viwili. Kipindi cha kwanza ni kuanzia Juni 2-15 mwaka huu wakati cha pili kinaanza Juni 23 mwaka huu na kumalizika Juni 28 mwaka huu.

Wakufunzi wanaotambuliwa na CAF watakaoendesha kozi hiyo ni Sunday Kayuni na Salum Madadi kutoka Tanzania, na washiriki watajigharamia kwa kila kitu. Baadaye CAF watatuma Mkufunzi mwingine kwa ajili ya mitihani.

ULIMWENGU, SAMATA WAJIUNGA STARS
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wametua Dar es Salaam leo (Mei 17 mwaka huu) mchana, na kujiunga moja kwa moja kwenye kambi ya Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo itafanyika kesho (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Washambuliaji hao wa Taifa Stars wamewasili saa 7.25 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo jana (Mei 16 mwaka huu) timu yao ya TP Mazembe ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya huko.

Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani kimepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyoanzia Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.

Naye Kocha Msaidizi wa Zimbabwe, Kalisto Pasuwa amesema hawaifahamu vizuri Taifa Stars lakini wamekuja kwenye mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni kwa ajili ya kushinda, na kuwataka washabiki wajitokeze kwa wingi kuona kiwango cha timu yake.

Milango kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana wakiongozwa na Joseph Odartei Lamptey itakuwa wazi kuanzia saa 6 kamili mchana, na tiketi zitapatikana katika magari maalumu uwanjani hapo.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 20,000 kwa VIP A.

Thursday, May 15, 2014

SAMATTA, ULIMWENGU KUTUA DAR SIKU MOJA NA WAZIMBABWETIMU ya soka ya taifa ya Zimbabwe inawasili usiku wa kuamkia Jumamosi (Mei 17 mwaka huu) ikiwa na msafara wa watu 27 kwa ajili ya mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2015 nchini Morocco Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo itatua saa 7.30 usiku kwa ndege ya Ethiopian Airlines na itafikia hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi, Dar es Salaam.

Zimbabwe itafanya mazoezi siku hiyo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili saa 10:00 jioni kwenye uwanja huo huo.

Wakati huo huo: Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanatarajiwa kuwasili Jumamosi mchana (Mei 17 mwaka huu) kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).

Washambuliaji hao watatokea moja kwa moja Sudan ambapo kesho (Mei 16 mwaka huu) TP Mazembe itacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya huko.

Ujio wa washambuliaji hao utafanya wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kuwa wamepatikana kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika ambalo fainali zake zitachezwa mwakani nchini Morocco. Mchezaji mwingine wa nje ambaye tayari ameripoti Stars ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini Qatar.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linamshukuru Mmliki wa TP Mazembe ambaye pia ni Gavana wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na Taifa Stars kwa vile mechi dhidi ya Zimbabwe ipo nje ya kalenda ya FIFA.

Naye Kocha Nooij atakuwa na mkutano na Waandishi wa habari kesho (Mei 16 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo katika hoteli ya Accomondia.

Wednesday, May 14, 2014

KABURU, JULIO WAJITOSA UCHAGUZI MKUU SIMBA


MAKAMU mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' na aliyekuwa akikaimu nafasi yake, Joseph Itang'are 'Kinesi' wamechukua fomu za kuwania nafasi ya makamu wa rais.

Kujitokeza kwa Kinesi na Kaburu kuwania nafasi hizo, kumeufanya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu uwe mgumu zaidi.

Kinesi alichukua fomu juzi wakati Kaburu alichukua fomu jana huku akisindikizwa na kundi kubwa la wanachama.

Kocha Msaidizi wa zamani wa Simba,Jamhuri Kihwelu 'Julio' naye amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya makamu wa rais huku akitamba kuwa, ana uwezo mkubwa wa kushika wadhifa huo.

Julio aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, anaifahamu vyema Simba na kuongeza kuwa, viongozi wengi waliowahi kuiongoza klabu hiyo ni wababaishaji.

Kinesi, Kaburu na Julio sasa watachuana na Sued Nkwabi na Badra Mayage katika kuwania wadhifa huo.

Katika nafasi ya rais, wagombea waliojitokeza hadi jana ni Evans Aveva, Michael Wambura na Andrew Tupa. Leo ndio siku ya mwisho kwa wagombea kuchukua na kurejesha fomu.

Kamati ya uchaguzi ya Simba inatarajiwa kukutana Mei 17 mwaka huu kwa ajili ya kuhakiki na kufanya mchujo wa wagombea. Majina ya wagombea watakaopitishwa yanatarajiwa kutangazwa Mei 19 mwaka huu.

Pingamizi kwa wagombea zitatolewa Mei 20 na 22 kabla ya kamati kuzipitia Mei 25 mwaka huu. Usaili kwa wagombea utafanyika Mei 29.

Tuesday, May 13, 2014

TFF YATUMA RAMBIRAMBI KIFO CHA MKUFUNZI WA WAAMUZI OMARI KASINDE

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mkufunzi wa waamuzi nchini, Omari Kasinde kilichotokea jana (Mei 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Mbali ya kuwa Mkufunzi, Kasinde ambaye anazikwa leo (Mei 13 mwaka huu) mchana katika Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyopita ya Waamuzi ya TFF iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Kapteni mstaafu Stanley Lugenge.

Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini kwani, Kasinde enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa katika mchezo huu tangu akiwa mwamuzi na baadaye mkufunzi na kiongozi..

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kasinde, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

KIINGILIO STARS NA ZIMBABWE BUKU TANO


Kiingilio cha chini cha mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.

Washabiki watakaolipa kiingilio hicho ni kwa wale watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.

Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mechi hiyo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, na uwanja siku ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij inatarajia kurejea jijini Dar es Slaam kesho (Mei 14 mwaka huu) kutoka Mbeya kuendelea na maandalizi ya kuikabili Zimbabwe.

MALINZI ATETA NA KLABU ZA LIGI KUU
Mkutano wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenyeviti wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kupata maoni yao juu ya changamoto zilizojitokeza katika ligi hiyo umefanyika juzi (Mei 11 mwaka huu).

Klabu za VPL zilizohudhuria mkutano huo ni Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Polisi Morogoro, Ndanda FC, Ruvu Shooting, Stand United na Tanzania Prisons.

Simba na Yanga hazikuhudhuria mkutano huo, na wala klabu hizo hazikutoa udhuru wowote wa kutokuwepo.

Maazimio ya mkutano huo ni kuwa kwa misimu mitatu ijayo kuanzia msimu wa 2014/2015, klabu zimekubaliana ziruhusiwe kusajili wachezaji watano wa kigeni. Kamati ya Utendaji ya TFF itatoa uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo katika kikao chake kijacho.

Pia klabu hizo zimekubali timu zao za U20 kuanzia msimu ujao zicheze ligi ya mkondo mmoja. Hata hivyo, utekelezaji wa hilo utategemea na upatikanaji wa mdhamini wa ligi hiyo ambapo TFF inafanya jitihada za kumpata mdhamini huyo.

Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake, Lina Kessy amezishauri klabu za VPL kuanzisha timu za wanawake, ambapo klabu hizo zimesema zitaufanyia kazi ushauri huo.

MBUYU TWITE AONGEZA MKATABA YANGAMlinzi kiraka wa timu ya Young Africans Mbuyu Junior Twite leo ameongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia klabu ya Yanga baada ya kufikia makubaliano na uongozi na kupata majibu ya Shirikisho la Soka nchini TFF juu ya idadi ya wachezaji wa kimataifa kwa msimu ujao 2014/2015.


Usajili wa Twite umefanyika leo makao makuu ya klabu ya Yanga chini ya Katibu Mkuu Bw Beno Njovu ambapo mchezaji amesema ataendelea kujitolea kwa uwezo wake kuisaidia timu yake ya Yanga.

Katibu Mkuu wa Young Africans Beno Njovu amesema wameingia mkataba wa mwaka mmoja na Twite baada ya pande zote kukubaliana, hivyo kuanzia sasa Twite ataendelea kuwa mchezaji wetu kwa msimu ujao wa 2014/2015 na kusisitiza kuwa usajili ndio umeanza sasa.

Akiongea mara baada ya kuweka sahihi kwenye mkataba wake mpya Twite amesema anajisikia furaha kuendelea kuwa mchezaji wa Yanga, kwani anafurahia maisha ya Jangwani, wapenzi, washabiki, viongozi na wachezaji ni marafiki/ndugu ndani na nje ya Uwanja.

Aidha Twite amesema Yanga ni miongoni mwa timu kubwa barani Afrika, zenye washabiki na waachama wengi hivyo wangu ni fahari kuendelea kuitumika timu hii ambayo tangu kujiunga nayo nimekua nikijtoa kwa moyo wangu wote kusaka mafanikio.

Mbuyu Twite amekua ni mchezaji wa Young Africans kwa kipindi cha miaka miwili tangu Julai 2012 alposajiliwa huku katika kipindi hicho chote akiwa ni mchezaji wa kikosi cha kwanza ambapo msimu uliopita aliweza kuisadia timu yake kutwaa Ubingwa wa Lig Kuu ya Vodacom na msimu huu kushika nafasi ya pili.

SERIKALI YAKIRI HAILINDI KAZI ZA WASANII, YATOA AGIZO KWA COSOTA NA TRA


SERIKALI imekiagiza Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), kukutana na uongozi wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini (TRA), ili kupanga mikakati ya kulinda kazi za wasanii.

Agizo hilo lilitolewa jana bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Mchemba alipokuwa akijibu swali la Martha Mlata (Viti Maalumu-CCM).

Katika swali lake la nyongeza, Martha alitaka kujua serikali imejipanga vipi kulinda kazi za wasanii kwa vile utaratibu wa sasa wa kuweka stempu za TRA umelenga zaidi kukusanya mapato.

Mchemba alikiri kuwa ni kweli kuweka stempu za TRA kwenye kazi za wasanii hakulengi kulinda kazi za wasanii zaidi ya kukusanya mapato ya serikali.

"Hivyo naiagiza COSOTA katika siku tano hizi zijazo, ikutane na TRA ili kupanga njia nzuri za kulinda kazi za wasanii na watuletee mrejesho ili tuone nini la kufanya,"alisema.

MBEYA CITY YAPANGWA KUNDI GUMU KOMBE LA NILE


WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya soka ya Kombe la Nile, Mbeya City wamepangwa kundi B pamoja na timu za El Merreikh al Fasher ya Sudan, Elman ya Somalia na AFC Leopards ya Kenya.


Taarifa iliyotolewa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) jana inaonyesha kuwa, michuano hiyo imepangwa kuanza Mei 22 mwaka huu mjini Khartoum, Sudan.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nchi zote wanachama wa CECAFA zimethibitisha kushiriki katika michuano hiyo, isipokuwa Eritrea. CECAFA inaundwa na nchi wanachama 11.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa kundi A litaundwa na timu za El Merreikh ya Sudan, SC Victoria Universty ya Uganda, Malakia ya Sudan Kusini na Polisi ya Zanzibar.

Kundi C litakuwa na timu za Al Ahli Shandi ya Sudan, Al Masry ya Misri, Defence ya Ethiopia na Dikhil ya Djibouti.

Kundi D litakuwa na timu za Hey Al Arab ya Sudan, Arab Contractors ta Misri, Flambeay de i'Est ya Burundi na Etincelles ya Rwanda.

Michuano hiyo itachezwa katika vituo vya Khartoum, Shandy na Red Sea (Port Sudan).

Katika mechi za ufunguzi, Victoria Universty itacheza na Malakia mjini Khartoum, El Merreikh itakipiga na Polisi wakati Arab Contractors itavaana na Flambeau mjini Port Sudan.

MECHI YA TAIFA STARS, ZIMBABWE SASA KUCHEZWA J'PILI DAR


Mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itafanyika Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Awali mechi hiyo tulipanga ichezwe Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kwa nia ya kuhakikisha mikoa yote ya Tanzania inapata fursa ya kuwa mwenyeji wa mechi za kimataifa.

Ili Uwanja wa Sokoine uweze kuchezwa mechi za kimataifa za mashindano, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilituma Mkaguzi (inspector) wake kwenye uwanja huo Jumamosi (Mei 10 mwaka huu) ambapo imeamua kuwa marekebisho yanayofanyika hayatamalizika katika muda stahili, hivyo mchezo huo kutochezwa Sokoine.

Tunatoa mwito kwa wamiliki wote wa viwanja kuwasiliana na TFF ili Idara ya Ufundi iwaelekeze maboresho ya kufanya ili viwanja vingi iwezekanavyo viweze kukidhi viwango vinavyotakiwa na CAF na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini mkoani Mbeya itarejea Dar es Salaam keshokutwa (Mei 14 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo.

Monday, May 12, 2014

DALALI AMPIGIA DEBE AVEVA


 MWENYEKITI wa zamani wa klabu ya Simba, Hassan Dalali (kulia) akipeana mkono na Aveva baada ya kumnadi kwa waandishi wa habari.
EVANS Aveva akisalimiana na mmoja wa wanachama wa klabu ya Simba kabla ya kuingia makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari.