KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 21, 2014

NGORONGORO HEROES YAENDA NIGERIA


Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) chenye watu 25 kinaondoka kesho alfajiri kwenda Nigeria kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).

Mechi hiyo itachezwa Jumamosi (Mei 24 mwaka huu) katika Jiji la Kaduna kwenye Jimbo la Kaduna ambalo lipo katikati ya Nigeria. Msafara wa timu hiyo unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi unaondoka kwa ndege ya Ethiopian Airlines.

Ngorongoro Heroes inayonolewa na Kocha John Simkoko ilipoteza mechi ya kwanza iliyofanyika nyumbani jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0.

Mwamuzi Alhadi Allaou Mahamat wa Tchad ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Atasaidiwa na Issa Yaya, Alfred Madjihoudel na Idriss Biani wote kutoka Tchad. Kamishna ni Aboubakar Alim Konate wa Cameroon.

TIMU YA U15 YAWASILI GABORONE
Timu ya Tanzania ya umri chini ya miaka 15 imewasili salama jijini Gaborone, Botswana kwa ajili ya michezo ya Afrika ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Mei 22 mwaka huu dhidi ya Mali.

Kikosi hicho cha wachezaji 16 chini ya Kocha Abel Mtweve kimetua jijini Gaborone jana (Mei 19 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South African Airways. Michezo hiyo itamalizika Mei 30 mwaka huu.

Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Tanzania ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.

Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland.

Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambazo nazo zilikuwa zishiriki kwenye michezo hiyo zimejitoa dakika za mwisho.

No comments:

Post a Comment