KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 11, 2014

REAL MADRID KUTUA DAR AGOSTI 23



KIKOSI cha wachezaji wakongwe wa timu ya Real Madrid kutoka Hispania, kinatarajiwa kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki na nyota wa soka wa Tanzania, mchezo utakaofanyika Agosti 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Kampuni ya TSN, Dennis Ssebo alisema jana kuwa, kikosi hicho kitaundwa na wachezaji nyota wa zamani, 'Real Madrid Legend Team', waliowahi kuwika katika timu hiyo.


Timu hiyo ya Real Madrid Legend iliwakilishwa na mchezaji mkongwe na kapteni wa timu hiyo, Ruben de la Red aliyeambatana na mchezaji mwingine mkongwe, Rayo Garcia pamoja na Isaac Recarey Sanchez,
anayehusika na maswala ya mahusiano ya Real Madrid Legend Club.

Akizungumza na wana habari, mwakilishi huyo wa TSN alisema timu hiyo itawakilishwa na wachezaji 25 na itakuwepo nchini kwa siku tatu ikiwa na ratiba ya kufanya shughuli mbalimbali.

"Nje ya mechi ya kirafiki na timu yetu ya Taifa, wachezaji hawa wakongwe ambao bado wako fiti na wanacheza soka, wanatazamiwa kutembelea mbuga za wanyama kwa minajili ya kuendelea kutangaza utalii wa Tanzania,"alisema.

Mwakilishi na kepteni wa timu ya Real Madrid Legend, aliishukuru kampuni ya TSN kwa kuwapa nafasi ya kuja kuiona Tanzania.

Alisema wanatambua kuwa Tanzania ni moja ya nchi yenye mashabiki wengi wa soka na anaamini mechi yao na vijana wa Tanzania itakuwa kali na mashabiki watakaohudhuria watafurahia.

Aliwashauri vijana wa timu ya Tanzania kuanza kujifua mapema kabla ya kukabiliana nao kwa kile alichodai kuwa, inawezekana baadhi yao hawachezi tena soka, lakini bado wako fiti na wembe mkali.

Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi aliipongeza kampuni ya TSN kwa hatua hii nzuri itakayoongeza tija kwa soka nchini, machoni mwa ulimwengu wa soka duniani na kuahidi kutoa ushirikiano kamili katika ujio huu.

“TSN wamefanya jambo la busara sana kwa soka nchini. Ujio wa timu hii utatupa mafunzo mengi na uzoefu walionao wachezaji hawa, lakini pia watasaidia kuitangaza nchi kwa ujumla. TFF inaahidi kutoa ushirikiano kamili kwa TSN ili kufanikisha ziara hii,” alisema.

TSN imesaini mkataba na wawakilishi wa Real Madrid leo katika hoteli ya Serena.

No comments:

Post a Comment