KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 24, 2013

IBRAHIMOVIC:OLE WAKO RONALDO



ZURICH, Uswisi
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic, amemchimbia mkwara nyota wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo.

Mkwara huo wa Ibrahimovic, unahusu pambano maalumu la michuano ya kuwania tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia kati ya Sweden na Ureno.

Ibrahimovic ameeleza kupitia waraka maalumu aliomwandikia Ronaldo kwamba, atahakikisha Sweden inashinda pambano hilo na kwenda Brazil kucheza fainali za michuano hiyo.

Mshambuliaji huyo wa Sweden amesema, hakutarajia iwapo Sweden ingepangwa kucheza na Ureno, hivyo ni jukumu la kila mmoja kati yao kuhakikisha anaisaidia timu yake.

"Naelewa kwamba watu wengi hawakupendi, lakini kamwe sijawahi kupatwa na hisia hizo kuhusu wewe. Siku zote nimekuwa nikikuona kama mtu dhaifu na haufanani na Zlatan kiuchezaji," ametamba nyota huyo wa Sweden.

Hata hivyo, Ibrahimovic amekiri kuwa, kwa vile hakutakuwa na wachezaji 11 wa Sweden wanaofanana na yeye kiuchezaji, hawezi kuwa na uhakika wa ushindi dhidi ya Ureno.

"Sweden haikufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2010. Haya hayakuwa mafanikio kwa Zlatan. Kama itatokea tena hivyo, nitalazimika kutumia njia nyingine ya kukufanya uonekane kama vile umehudhuria hafla, ambayo Lionel Messi alikushinda katika kila kipengele,"ameeleza kupitia waraka huo.

"Hili si tishio. Zlatan hatoi vitisho. Ninazungumzia vitu ambavyo huwa vinatokea. Fainali za Kombe la Dunia zinamuhitaji Zlatan,"amesisitiza Ibrahimovic.

"Nakutakia kila la heri Cristiano, lakini baada ya kusoma haya, sidhani kama utaihitaji. Kama unadhani Pepe anaweza kukulinda kwa Zlatan, umekosea na utalia," aliongeza nyota huyo wa Sweden.

"Huenda baada ya pambano hili kumalizika, tutakuwa marafiki. Nitakuona uwanjani na utaniona kwenye ndoto zako,"ameeleza nyota huyo.

No comments:

Post a Comment