KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 20, 2013

TFF YAIONYA YANGA



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewaonya viongozi, wanachama na mashabiki wa Yanga kuepuka kuwazuia wafanyakazi wa kituo cha televisheni cha Azam kuonyesha pambano lao la ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, kituo cha televisheni cha Azam kimepewa haki kisheria ya kuonyesha mechi zote za ligi hiyo, zikiwemo zinazoihusu Yanga.

Angetile amesema wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa, wafanyakazi wa kituo hicho, hawapati bughudha yoyote wakati wakitimiza majukumu yao kwenye viwanja vinavyotumika kwa mechi za ligi hiyo.

Onyo hilo la TFF kwa Yanga limekuja siku chache baada ya viongozi na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, kuwazuia wafanyakazi wa Azam wasichukue picha za pambano kati ya timu hiyo na Mtibwa Sugar lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

"Tutaweka ulinzi wa kutosha kwa wafanyakazi wa Azam televisheni na kuhakikisha wanatimiza majukumu yao bila kubughudhiwa,"alisema.

Angetile alionya kuwa, mtu yeyote atakayewazuia wafanyakazi hao kutekeleza majukumu yao, mbali ya kukamatwa, atachukuliwa hatua za kisheria kwa kufikishwa mahakamani.

Kituo cha televisheni cha Azam kimeingia mkataba wa miaka mitatu wa kuonyesha mechi za ligi hiyo laivu. Kituo hicho kimeshalipa sh. bilioni 5.56 kwa ajili ya kutekeleza mkataba.

Kwa mujibu wa mkataba huo, kila timu itapata mgawo wa sh. milioni 100 kwa msimu mmoja na tayari timu 13 kati ya 14 zimeshapata sehemu ya fedha hizo, ambazo ni sh. milioni 25 kila moja.
Yanga ndiyo timu pekee iliyogomea mkataba huo na kutochukua mgawo wake wa sh. milioni 25 kwa madai kuwa, mkataba huo hauna manufaa kwa klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment