KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 1, 2013

YANGA YAUMBUKA, ENEO LA JANGWANI KUJENGWA CITY GARDEN, YADAIWA FEDHA ZA KODI YA ARDHI



SERIKALI imesema klabu ya Yanga haiwezi kupewa eneo la ziada kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wake wa kisasa wa soka.

Ofisa Habari wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rehema Isengo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari eneo la Jangwani liko katika mipango ya maendeleo.

Msimamo huo wa wizara huenda ukawa pigo kubwa kwa Yanga, ambayo ilipanga kujenga uwanja wa kisasa katika maeneo ya Jangwani, Dar es Salaam.

Mbali na kujenga uwanja wa kisasa, Yanga pia ilipanga kujenga maduka, hoteli, viwanja vya mazoezi, ukumbi wa mikutano na eneo la kuegesha magari.

Klabu hiyo, juzi ilsitisha mkataba wa ujenzi wa uwanja huo na Kampuni ya Beijing Contractors Engineering ya China, ikisubiri majibu ya barua yao ya kupata eneo la nyongeza kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Rehema alisema katika mazungumzo ya awali kati ya wizara na manispaa, tayari eneo la Jangwani liko kwenye mradi wa kujengwa City Garden, hivyo Yanga haiwezi kupewa eneo hilo.

Alisema Yanga ilishapewa majibu hayo kupitia ofisi ya mipango miji na kuongeza kuwa, wizara haihusiki na ugawaji wa viwanja kwa vile suala hilo lipo chini ya halmashauri. Alisema kazi ya wizara ni kupitia faili lililowasilishwa kabla ya kutia saini.

Mbali na hilo, Rehema alisema Yanga inadaiwa deni la kodi ya ardhi tangu mwaka 1997 hivyo ameitaka kulilipa mara moja.

"Yanga siyo walipaji wazuri wa kodi, wanadaiwa kodi tangu 1997, wameshapewa maelezo wafuatilie na kulipa kodi hiyo,"aliongeza.

Ofisa Habari huyo aliweka wazi kuwa, athari inazoweza kupata Yanga endapo itashindwa kulipa deni hilo ni kunadiwa kwa mali zake au kupelekwa mahakamani.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo jana.

No comments:

Post a Comment