SIKILIZENI vijana. Nataka ushindi. Sitaki kusikia mnafungwa ama kutoka sare.Hivi ndivyo Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji alivyokuwa akiwaambia nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' na msaidizi wake, Athumani Iddi 'Chuji' wakati wa mazoezi ya gym yaliyofanyika jana kwenye jingo la Quality Centre, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Manji akiteta jambo na mshambuliaji Mrisho Ngasa wakati wa mazoezi ya gym yaliyofanyika jana kwenye jingo la Quality Centre.
MSHAMBULIAJI Didier Kavumbagu wa Yanga jana aligoma kufanya mazoezi na wachezaji wenzake kutokana na uongozi wa klabu hiyo kupuuza madai yake.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Burundi kodi ya nyumba anayoishi imemalizika na hana pesa zingine za kulipa.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, Kavumbagu aliwaeleza tatizo hilo viongozi wa Yanga tangu wiki iliyopita, lakini wamekuwa wakimpuuza.
"Hali hiyo ndiyo iliyosababisha Kavumbagu ashindwe kuja mazoezini leo," kilieleza chanzo hicho cha habari.
Wachezaji wa Yanga jana walipelekwa kufanya mazoezi kwenye gym iliyoko kwenye jengo la Quality Centre lililoko barabara ya Nyerere mjini Dar es Salaam.
Kavumbagu amekuwa mchezaji wa pili kutoka nje kugoma kufanya mazoezi na timu hiyo wiki hii. Wengine ni beki Mbuyu Twite na kiungo Haruna Niyonzima.
Twite amegoma kufanya mazoezi kutokana na uongozi wa Yanga kushindwa kumtafutia nyumba ya kuishi na kumlipia kodi kama alivyoomba kwa uongozi wiki iliyopita.
Kwa upande wake, Niyonzima amegoma kufanya mazoezi kutokana na uongozi kushindwa kummalizia pesa zake za usajili. Hata hivyo, haijajulkana kiwango cha pesa anazodai mchezaji huyo.
Mmoja wa watendaji wapya wa Yanga, Patrick Naggi alisema jana kuwa, ni kweli Twite na Kavumbagu wana matatizo ya nyumba za kuishi, lakini hakueleza tatizo hilo litatatuliwa lini.
Hata hivyo, Naggi alisema Niyonzima hajagombea mazoezi, isipokuwa amepatwa na matatizo nchini Rwanda, ambako imedaiwa kuwa, mmoja wa watoto wake amepotea.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji amewataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanashinda mechi zao zijazo za ligi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.
Manji alitoa agizo hilo jana alipozungumza kwa faragha na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' na msaidizi wake, Athumani Iddi 'Chuji' wakati wa mazoezi ya gym yaliyofanyika kwenye jengo la Quality Centre.
Alisema hataki kuona timu hiyo ikifungwa ama kutoka sare kwa sababu matokeo ya aina hiyo yatawaweka kwenye mazingira magumu ya kutetea ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Mwenyekiti huyo wa Yanga amewataka wachezaji kuwa na umoja na kucheza kwa ushirikiano ili waweze kutimiza malengo yao.
Yanga inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi sita. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 14 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
No comments:
Post a Comment