KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 10, 2013

ABDALLA KIBADENI: SICHEZESHI MCHEZAJI SABABU YA UMAARUFU



LICHA ya timu kongwe ya soka nchini, Simba kuongoza katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, baadhi ya mashabiki hawajaridhishwa na mwenendo wake katika ligi kutokana na kulazimishwa kutoka sare katika mechi nyingi na kupata ushindi katika mechi chache. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kocha huyo anaelezea mambo mbalimbali kuhusu mwenendo wa timu hiyo.

SWALI: Umeiongoza Simba katika mechi saba za ligi kuu ya Tanzania Bara hadi sasa na mnaongoza kwa kuwa na pointi 15. Kipi ulichokiona kwa timu yako hadi sasa?
JIBU: Namshukuru Mungu kwamba hadi sasa tunaongoza ligi kwa tofauti ya pointi tatu kati yetu na Yanga. Binafsi namshukuru Mungu, viongozi wa klabu, benchi la ufundi, wachezaji na wanachama kwa kutuunga mkono na kuonyesha mshikamano mkubwa kwa timu yao.
Japokuwa hatujawa na mwenendo wa kuridhisha sana, lakini nina imani tutaweza kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo iwapo umoja na mshikamano uliopo sasa utaendelea kudumu.
Ninachopenda kuwatahadharisha wana-Simba wote ni kwamba, waendelee kuwa na uvumilivu kwa sababu timu yao ni mpya na iwapo watagawanyika, mambo yanaweza kuharibika.
SWALI: Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na malalamiko kwako kuhusu upangaji wa timu. Inadaiwa kwamba, umekuwa ukipenda kuwapanga baadhi ya wachezaji  wakati uwezo wao ni mdogo. Kuna ukweli wowote kuhusu malalamiko haya?
JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba, kila mtu ana uhuru wa kuzungumza lolote analotaka kutokana na vile anavyofikiria. Lakini jambo la msingi ni kwamba, mimi ni kocha mwenye taaluma na ndiyo inayoniongoza katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku.
Siwezi kwenda kinyume na mafundisho niliyopewa wakati nikisomea kazi hii, ikiwa ni pamoja na kuzingatia uwezo wa mchezaji katika upangaji wa timu, afya yake na mambo mengine muhimu ya kiufundi.
Mchezo wa soka una mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kufahamu kila kitu kinachomuhusu mchezaji wako ndani ya saa 24, iwapo ana matatizo ama anasumbuliwa na jambo lolote linaloweza kumtoa mchezoni. Ni lazima kocha afahamu yote haya kabla ya kuamua kumpanga mchezaji kwenye timu.
SWALI: Kuna tuhuma kwamba kikosi chako kimegawanyika kutokana na kuwepo kwa shinikizo la kupangwa kwa baadhi ya wachezaji kutoka kwa viongozi na wadau wa Simba. Kuna ukweli wowote kuhusu tuhuma hizi?
JIBU: Sidhani kama kuna ukweli wowote kuhusu tuhuma hizo. Kama ingekuwa ni kweli, sidhani iwapo tungeweza kuongoza ligi hadi sasa. Watu wanaoeneza tuhuma hizo, hawana nia njema na Simba na bila shaka wana malengo yao.
Ninachoweza kusema ni kwamba, kwa sasa Simba imetulia na kazi inaendelea kufanyika kwa umakini mkubwa, ingawa yapo matatizo ya hapa na pale ya kiufundi, ambayo hayawezi kukosekana, lakini ninapambana nayo.
SWALI: Ni matatizo yepi, ambayo umekuwa ukikumbana nayo kwa sasa?
JIBU: Matatizo yapo mengi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la wachezaji majeruhi na wengine kucheza chini ya kiwango. Mchezaji anapokuwa katika hali hiyo, ninalazimika kumweka pembeni kwenye programu yangu.
Tatizo ni kwamba, mashabiki wengi hawaelewi mambo haya ndio sababu wanapoona mchezaji hapangwi, wanaanza kulalamika na kuhoji na pengine kulitupia lawama benchi la ufundi.
Lakini kwa ujumla ni kwamba ninashirikiana vyema na viongozi kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa na afya njema na hali nzuri ya kuwawezesha kuitumikia timu yao kila kukicha. Hakuna kitu kinachoitwa kuwapendelea baadhi ya wachezaji. Mchezaji atachezeshwa kutokana na bidii yake na kujituma kwake.
SWALI: Tatizo lipi kubwa umeliona katika ligi hadi sasa?
JIBU: Tatizo kubwa lililopo na ambalo nadhani ni sugu, ni uchezeshaji mbovu wa baadhi ya waamuzi. Baadhi ya waamuzi wamekuwa hawaitendei haki timu yetu na jambo hili limekuwa likiwavunja nguvu wachezaji.
Waamuzi wengine wanafanya hivyo kutokana na kushindwa kuzitafsiri vyema sheria 17 za soka, lakini wengine wanafanya makusudi kwa sababu, ambazo hazieleweki.
SWALI: Umeshapata kikosi cha kwanza cha Simba baada ya kuwa umeiongoza katika mechi saba za ligi?
JIBU: Kusema ule ukweli, hadi sasa Simba haijawa na kikosi cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali. Mojawapo ya sababu hizo ni kuendelea kupima uwezo wa kila mchezaji kutokana na ukweli kwamba wengi ni wapya na hawajazoeana sawasawa.
Huenda baada ya kufikisha mechi 10, nitakuwa nimepata kikosi cha kwanza kwa vile wachezaji watakuwa wamecheza mechi nyingi na kuzoea mikikimikiki ya ligi. Lakini kwa sasa bado kutokana na ugeni wa wachezaji kwenye timu. Tunachokifanya kwa sasa ni kuunganisha mfumo wa uchezaji kutokana na staili ya kila mchezaji.
Tunao wachezaji wapya watatu kwenye timu kutoka nje, Gilbert Kaze, Hamisi Tambwe na Joseph Owino, ambao hawana muda mrefu kwenye timu na wengine tumewapandisha kutoka kikosi cha pili. Lengo letu ni kuwa na kikosi imara na cha ushindi.
SWALI: Unapenda kuwaeleza nini mashabiki wa Simba?
JIBU: Nawaomba watulie na wafahamu kwamba, timu yao inapita kwenye kipindi kigumu kutokana na uwepo wa wachezaji wengi wapya. Itachukua muda kidogo kwa timu yao kuwa imara zaidi hivyo uvumilivu ni kitu muhimu.
Huwezi kumlaumu kocha baada ya kuwa na timu kwa miezi michache na isitoshe tunafanya jitihada kubwa za kuifanya Simba iwe tishio ndio sababu unaona tunaongoza ligi na wapinzani wetu wapo nyuma yetu.

No comments:

Post a Comment