'
Thursday, October 24, 2013
MALINZI ATANGAZA NEEMA TFF
MGOMBEA wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amesema itamchukua siku 100 kuleta mabadiliko ya uendeshaji wa mchezo huo.
Malinzi alisema hayo mjini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizindua kampeni za uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika Jumapili.
Alisema iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, atahakikisha vipaumbele vyote alivyoviweka, vinafanyiwa kazi ili kuleta mageuzi katika mchezo huo.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendeleza soka kwa vijana, makocha, vifaa vya michezo na uboreshaji wa viwanja.
Malinzi alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuendeleza utulivu ndani ya TFF, kubuni na kuboresha ustawi wa soka nchini na kuunda upya idara ya ufundi iliyoko ndani ya shirikisho hilo.
Alisema anataka idara hiyo iwe kichocheo kikubwa katika maendeleo ya soka nchini na itatengewa fedha nyingi kuliko idara zingine kutokana na umuhimu wake.
Kwa mujibu wa Malinzi, vipaumbele vyake vingine ni kujenga kituo kipya cha soka, kitakachokuwa na uwanja wa kisasa, vituo vya tiba, maabara za utafiti na hosteli za wanamichezo.
Malinzi alisema pia kuwa, atahakikisha ligi kuu ya Tanzania Bara, inakuwa na timu nyingi, tofauti na ilivyo sasa na waamuzi wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kwenda na wakati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment