'
Thursday, October 10, 2013
EVRA AMUOTA POGBA
LONDON, England
NAHODHA Msaidizi wa Manchester United ya England, Patrice Evra, amekiri klabu hiyo ilifanya kosa kubwa kumpiga bei mshambuliaji wake kinda, Paul Pogba.
Pogba, amejiunga na klabu ya Juventus ya Italia na amekuwa chaguo la kwanza la Kocha Antonio Conte, baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika michuano ya Ligi Kuu ya Italia.
Evra amesema lilikuwa kosa kubwa kumtoa Pogba katika kikosi chao kwani ni mshambuliaji mwenye kipaji cha kufunga mabao na alikuwa bado muhimu kwa Mashetani Wekundu.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 20, aliondoka Manchester United mwaka jana katika mazingira ya kutatanisha baada ya kutibuana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson.
Wachezaji nguli wa Manchester United, Ryan Giggs na Paul Scholes ni miongoni mwa nyota waliotaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa abaki Old Trafford.
"Ana kipaji uwanjani, ni mahiri na anajua mpira. Ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kama walivyo Ryan Giggs na Paul Scholes," amesema nahodha huyo wa zamani wa Ufaransa.
Katika moja ya mazungumzo na vyombo vya habari vya Ufaransa, Pogba, alidokeza kuwa, aliwahi kumwambia Ferguson ampange na atamuonyesha vitu vyake uwanjani, lakini alimpuuza.
"Desemba 31, 2011 katika mchezo wetu dhidi ya Blackburn, nilikuwa kwenye benchi, nilishangaa Ferguson alimpanga Rafael na Ji Sung Park kucheza kiungo, nilichukia sana," alisema Pogba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment