KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 24, 2013

TCHETCHE, BALOU MAPACHA WA IVORY COAST WANAOIBEBA AZAM


KIPRE Tchetche na Kipre Balou ni wanasoka wawili mapacha kutoka Ivory Coast wanaocheza soka ya kulipwa katika klabu ya Azam, inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Mapacha hao ni miongoni mwa wanasoka wa kigeni wanaolipwa fedha nyingi na klabu za Tanzania, wakiwemo wengine wanaotoka katika nchi za Kenya, Burundi na Uganda.

Tchetche na Balou walichangia kwa kiasi kikubwa kuiwezesha Azam kushika nafasi ya pili katika ligi kuu msimu uliopita na kupata tiketi ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika michuano ya Kombe la Shirikisho na kuishia raundi ya tatu.

Tchetche alikuwa wa kwanza kutua nchini Januari 2011 baada ya kuivutia Azam wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji, iliyofanyika Desemba 2010. Ivory Coast ni miongoni mwa timu zilizoalikwa kushiriki kwenye michuano hiyo.

Baada ya kuichezea Azam kwa msimu mmoja, Tchetche alivutiwa na michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara na kuamua kwenda nyumbani, ambapo aliporejea, alimchukua pacha wake Balou.
Akiwazungumzia wachezaji hao, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall alisema ni wa kiwango cha juu.

"Tumepata thamani halisi ya pesa. Tchetche na Balou wameongeza thamani katika timu yetu,"alisema Hall.

Tchetche aliifungia Azam mabao 20 msimu uliopita, 17 katika ligi kuu ya Tanzania Bara na mengine matatu katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Kwa upande wake, Balou ni kiungo mkabaji japokuwa wakati mwingine amekuwa akipanda mbele kusaidia mashambulizi.

Stewart hakuwa tayari kutaja kiwango cha fedha wanacholipwa wachezaji hao katika mikataba yao, lakini alisisitiza kuwa, klabu imefaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na usajili wao.

"Hatukupata matatizo kuwapata na hawakutugharimu fedha nyingi,"alisema kocha huyo, ambaye ni raia wa Uingereza.

Kwa mujibu wa Stewart, machafuko yaliyotokea nchini Ivory Coast yalichangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wachezaji hao waje kutafuta pesa Tanzania kupitia mchezo wa soka.

"Kwa sababu kulikuwa na machafuko Ivory Coast na klabu za huko hazikuwa na fedha, hawakuwa na lingine la kufanya. Walihitaji pesa,"alisema Stewart.

Akizungumzia ligi kuu ya Tanzania Bara, Tchetche alisema ni ngumu ikilinganishwa na ile ya Ivory Coast, ina ushindani na wachezaji wanatumia nguvu.

"Ligi ina ushindani mkubwa na imetupa changamoto tofauti," alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26.

"Azam inatutunza vyema na tunayo mikataba mizuri. Siwezi kuzungumzia mshahara wangu, lakini tunajisikia tupo nyumbani,"alisema Tchetche.

Tchetche alisema aliporudi nyumbani Ivory Coast, alimweleza Balou kuhusu ligi ya Tanzania na klabu ya Azam na alikubali kuja naye nchini.

"Nilimweleza pacha wangu kwamba Azam ni klabu kubwa Tanzania na imekuwa ikifanya vizuri kadri siku zinavyosonga mbele na alikubali kuja nami,"alisema Tchetche.

Kabla ya kuja nchini, Tchetche alikuwa akichezea klabu ya JAC ya Ivory Coast wakati Balou alikuwa akichezea klabu ya Sewe Sport. Pia waliiwakilisha Ivory Coast katika michuano ya Kombe la CHAN kwa wachezaji wa ndani.

Tchetche na Balou wanaamini kuwa, Tanzania ni kama kituo cha muda katika harakati zao za kutaka kwenda kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya.

"Ndoto zetu ni kucheza katika ngazi za juu zaidi, hatuelewi ni lini mipango hiyo itafanikiwa, lakini hatuna haraka kwa sababu tunafurahia kuwepo hapa,"alisema Balou.

Tayari mapacha hao wameshazoea mazingira ya Tanzania na wameshaanza kufanya jitihada za kujifunza lugha ya kiswahili. Kwa ujumla, wanafurahia maisha ya Tanzania.

Azam, inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa Tanzania, Salim Bakhresa, imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya kuwekeza katika soka, ikiwa ni pamoja na kujenga uwanja wa kisasa eneo la Mbagala-Chamazi, Dar es Salaam.

Hivi karibuni, Azam ilianzisha kituo chake cha televisheni, ambacho kimeshapata idhini ya kuonyesha laivu mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara, inayoendelea katika viwanja mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment