'
Thursday, October 10, 2013
RAIS BIYA AMREJESHA ETO'O KIKOSI CHA CAMEROON
YAOUNDE, Cameroon
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto'o ameamua kubadili uamuzi wake wa kustaafu kucheza soka ya kimataifa.
Kutokana na uamuzi wake huo, Eto'o sasa ataichezea Cameroon katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 dhidi ya Tunisia.
Uamuzi huo wa Eto'o umekuja baada ya Rais wa Cameroon, Paul Biya, kuingilia kati na kumtaka mshambuliaji huyo kubadili msimamo wake wa kustaafu soka ya kimataifa.
Mshambuliaji huyo mpya wa Chelsea alikutana na wawakilishi wa Rais Biya, mjini Yaounde hivi karibuni kwa ajili ya kujadili mustakabali wake wa soka ya kimataifa.
Baada ya kikao hicho, Eto'o, alikubali kuendelea kuichezea Cameroon na alitarajiwa kuungana na wachezaji wenzake jana walioko kambini katika mji wa Nice nchini Ufaransa.
Pambano kati ya Cameroon na Tunisia, limepangwa kuchezwa Oktoba 13 mwaka huu mjini Rades kabla ya kurudiana Novemba 17 mjini Yaounde.
"Unaweza kupatwa na matatizo yote duniani, lakini unapaswa kuweka sawa mipango yako," alisema Eto'o juzi alipozungumza na redio ya taifa ya Cameroon.
"Huu ni wakati wa kuungana na wachezaji wenzangu nchini Tunisia na kurejea na matokeo mazuri,"aliongeza.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32, hivi karibuni aliwaambia wachezaji wenzake kwamba, angestaafu kuichezea timu ya taifa baada ya Cameroon kuifunga Libya.
Licha ya kuwepo kwa taarifa za kustaafu kwake, Kocha Mkuu wa Ujerumani, Volker Finke amemwita kwenye kikosi chake kitakachomenyana na Tunisia.
Katika siku zilizopita, Eto'o amekuwa na uhusiano mbovu na viongozi wa Chama cha Soka cha Cameroon, ikiwemo kuongoza mgomo wa wachezaji mwaka 2011 uliosababisha kufutwa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria.
Kufuatia mgomo huo, Eto'o alifungiwa kucheza mechi 15, lakini adhabu hiyo ilipunguzwa na kuwa mechi nane baada ya kukata rufani.
Hata baada ya kumalizika kwa adhabu hiyo, Eto'o aligoma kuichezea Cameroon kwa miezi kadhaa.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Biya kuingilia kati kumzuia mchezaji asistaafu soka. Mara ya kwanza alimshawishi Roger Milla arejee kuichezea Cameroon katika fainali za Kombe la Dunia za 1990 zilizofanyika Italia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment