'
Monday, October 28, 2013
MALINZI AWASAMEHE WAFUNGWA WOTE WA SOKA, ISIPOKUWA WATOA RUSHWA NA WAPANGAJI WA MATOKEO
RAIS mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ametoa msameha kwa wanachama wote wa shirikisho hilo waliofungiwa chini ya Utawala wa rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga, isipokuwa tu wale ambao adhabu zao zinatokana na makosa ya rushwa na kupanga matokeo.
Maana yake- Michael Richard Wambura aliyekwama kabisa kugombea nafasi yoyote chini ya utawala wa Tenga, sasa yuko huru kugombea au kuteuliwa kwa nafasi yoyote ya uongozi katika soka ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliomalizika usiku wa manane jana ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Malinzi aliiagiza Sekretarieti ya TFF chini ya Katibu wake, Angetile Osiah mara moja kuandika barua za misamaha kwa wote wanaotumikia adhabu za utawala wa Tenga.
“Hata rais wa nchi anapoingia madarakani huwa anatoa misamaha, nami nachukua fursa hii kuomba ridhaa yenu Wajumbe, kwa kuwa huu ni uongozi mpya, basi tufungue ukurasa mpya, nipeni ridhaa yenu, watu wote waliofungiwa chini ya utawala uliomaliza muda wake, wasamehewe tuanze upya. Isipokuwa wale tu ambao adhabu zao zinatokana na rushwa na upangaji matokeo,”alisema Malinzi.
Malinzi alisema muda si mrefu atakutana na Kamati yake ya Utendaji kujipanga na amewataka wajumbe wote kujiandaa kwa hilo.
Kwa upande wake, Tenga pamoja na kumpongeza Malinzi, aliahidi kumkabidhi ofisi Jumamosi ijayo.
Malinzi ameshinda Urais wa TFF baada ya kupata kura 72, dhidi ya 52 za mpinzani wake Athumani Jumanne Nyamlani.
Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Walace Karia alifanikiwa kushinda nafasi ya Makamu wa Rais kwa kupata kura 67 akiwashinda Nassib Ramadhani kura 52 na Imani Madega sita.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment