KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 10, 2013

DIAMOND ATABIRI KIFO CHAKE, ATUNGA WIMBO KAMA WA MAREHEMU KANUMBA



SIKU chache kabla ya kifo chake, aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba alitunga wimbo kuhusu kifo. Wimbo huo ulikuwa ukizungumzia mambo mbalimbali, ambayo alitabiri kwamba yatatokea baada ya kifo chake.

Hazikupita siku nyingi, Kanumba alifariki dunia baada ya kujigonga ukutani, nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam, baada ya kutokea ugomvi kati yake na msanii mwenzake, Elizabeth Michael 'Lulu'.

Wimbo huo, uliopigwa kwa miondoko ya taratibu, uliacha maswali mengi miongoni kwa mashabiki wake. Lakini kikubwa ni kwamba, Kanumba alijitabiria kifo chake kwa njia ya wimbo.

Wakati mashabiki wakiwa bado na kumbukumbu ya kifo hicho cha Kanumba, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond', naye ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Kama nikifa kesho.

Diamond amerekodi kibao hicho siku chache baada ya kuzindua wimbo wake wa My Number One, ambao bado unaendelea kutamba kwenye vituo mbalimbali vya redio na luninga nchini.

Msanii huyo machachari amepiga kibao hicho kwa miondoko ya taratibu, mipigo yake ikiwa haina tofauti kubwa na ile ya wimbo wake wa Kesho. Isipokuwa kibao hicho kimesheheni mashairi yanayohuzunisha.

Katika kibao hicho, Diamond anahoji iwapo atakufa kesho, nani atakayezikwa naye
na je, ni nani atakayembembeleza mama yake mzazi asilie.

"Ni swali gumu sana nauliza, lakini wakati utafika nitapumzishwa. Siku zamu yangu ikifika, nikiitwa na Mungu, uhai wangu utakatishwa. Nafsi yangu itatenganishwa na roho, milele nitakwenda kupumzika. Sijui wengi watalia kwa uchungu au watafurahi,"anaimba Diamond katika moja ya beti za wimbo huo.

Msanii huyo anakwenda mbali zaidi kwa kuhoji, baada ya kifo chake, wasanii wenzake watamwimbia au jina lake litafutika na nyimbo zake hazitasikika tena?

Kana kwamba haitoshi, Diamond anauliza iwapo wacheza shoo wa kundi lake la Wasafi watamlilia na kama ndugu na rafiki zake watahudhuria mazishi yake au atakapokufa atakuwa hana chake?

Diamond pia anamuusia mama yake mzazi akimweleza kuwa,hana mtoto hata wa kusingiziwa, hivyo wasije wakatokea mabinti wakamdanganya kwamba amezaa nao.

"Mama mwanao sina mtoto hata wa kusingiziwa,wengi tulipanga kufanya hivyo, lakini walisema wakati wao wa kuzaa bado. Nikiondoka wasikudanganye, waliniambia ngoja ngoja, wataharibu ujana wao, baada ya shida zao wakanikimbia,"ameimba Diamond.

Akizungumzia kibao hicho, Diamond ameeleza kupitia tovuti yake juzi kuwa, hakupanga kuutoa hivi karibuni na ameshangazwa na kitendo cha mtu, aliyeuvujisha kwenye mtandao.

"Kuvujisha wimbo wangu hakuwezi kunipunguzia wala kunidhuru chochote. Sanasana utanizidishia umaarufu na kunipa shoo zaidi,"ameeleza Diamond kupitia mtandao wake.

"Kama nimeacha kurekodi nyimbo kwenye studio yako, usipaniki, tulia, tafuta msanii mwingine mkali zaidi yangu umrekodie ngoma, apae juu kuliko mimi. Lakini kuvujisha nyimbo zangu, unajisumbua bure," ameongeza.

Katika hatua nyingine, Diamond amesema hajatengana na mpenzi wake wa sasa, Penny na kurudiana na mpenzi wake wa zamani, Wema Sepetu.

Diamond amesema taarifa zilizosambazwa na vyombo vya habari kwamba ametengana na Penny ni za uongo na uzushi.

"Kumekuwa na uvumi na habari nyingi sana mitandaoni na kwenye media tofauti kwamba mimi na mwanadada Wema Sepetu tuna uhusiano wa kimapenzi, kitu ambacho si kweli. Taarifa hizo ni za uongo," ameeleza.

Kwa mujibu wa Diamond, uvumi huo ulianza baada ya Wema kuchangia mada kwenye akaunti yake ya instagram.

"Hebu tujifunze kubadilika. Ina maana watu mkiwa hamko kwenye uhusiano wa mapenzi, basi msizungumze ama kushiriki katika jambo lolote? Futeni huo uzamani na mbadilike. Ina maana mnapenda kuona watu wana uadui? Ni muda wa kufanyakazi ili kulipa sifa na heshima Taifa la Tanzania na si kujengeana chuki zisizo na faida," ameeleza na kusisitiza anampenda Penny na hajarudiana na Wema.

Diamond ndiye msanii anayeongoza kwa kulipwa fedha nyingi kwa kila onyesho. Msanii huyo amekuwa akilipwa dola za Marekani 10,000 (sh. milioni 16) anapofanya onyesho moja nje ya nchi.

Katika mahojiano na vyombo vya habari hivi karibuni, Diamond alisema katika baadhi ya nchi, kiwango cha malipo kwa kila onyesho ni kati ya dola 15,000 (sh. milioni 24) na 25,000 (sh. milioni 42).

"Sifanyi shoo nje ya nchi chini ya dola 10,000. Katika nchi kama vile Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), kiwango changu ni dola 25,000. Wakati mwingine nalipwa hadi dola 30,000," alisema.

Diamond anasema kwa nchi kama vile Comoro, ambako alikwenda kufanya onyesho hivi karibuni, malipo kwa onyesho yalikuwa dola 25,000 (sh. milioni 42).

Hata hivyo, Diamond anasema wakati mwingine amekuwa akilipwa zaidi ya anavyotarajia, akitoa mfano wa Rwanda, ambako promota aliyemwalika alimlipa sh. milioni 180.

Kabla ya kujitosa katika muziki, Diamond aliwahi kufanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza mikoba kilichoko Mikocheni, Dar es Salaam kati ya 2008 na 2009 na kulipwa mshahara wa sh. 2,000 kwa saa nane.

Anasema mshahara huo ulikuwa mdogo, haukuweza kukidhi mahitaji yake ya kila siku kwa sababu alikuwa akitumia sh. 1,000 kwa nauli na sh. 1,000 kwa ajili ya chakula.

Diamond anamiliki vitega uchumi kadhaa, ambavyo ni hoteli, nyumba, viwanja, magari na pikipiki anazozitumia kwa biashara. Anasema mali hizo zina thamani ya sh. bilioni moja.

No comments:

Post a Comment