KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 20, 2013

KING MAJUTO; NATAKA UBUNGE NIWASAIDIE WANANCHI, ASEMA HANA NJAA, ANAZO FEDHA ZA KUTOSHA KUISHI VIZURI


MSANII nyota wa vichekesho na filamu nchini, Amri Athumani 'King Majuto' amesema, atagombea ubunge katika jimbo la Tanga Mjini katika uchaguzi mkuu ujao wa rais na wabunge, unaotarajiwa kufanyika 2015.

Akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM wiki hii, Majuto alisema amepanga kuwania ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM.

Mkongwe huyo wa sanaa nchini alisema, yeye ni muumini mzuri wa CCM na kwamba anakipenda na kukiheshimu kutokana na mfumo wake mzuri wa uongozi.

Majuto (60) alisema ameamua kujitosa kwenye siasa ili kuendeleza mafanikio, ambayo wasanii wa fani mbalimbali nchini wameyapata baada ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Msanii huyo mkongwe alisema, anaamini kuwa, uzoefu alioupata kutokana na kuishi Tanga kwa miaka mingi, utamwezesha kutatua matatizo na kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.

"Lengo langu ni kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wenzangu iwapo Mungu atanisaidia katika kusudio langu hili,"alisema.

Majuto alisema hali ya sasa ya Tanga na ugumu wa maisha ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya aamue kujitosa kwenye ulingo wa siasa kwa kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Kwa sasa, mbunge wa jimbo la Tanga Mjini  ni Omar Nundu, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Uchukuzi.

"Wakazi wengi wa Tanga wamekuwa wakiishi maisha magumu na ya kukatisha tamaa, hivyo wakati umefika wa kujitosa kwenye siasa ili kuwasaidia wawe na maisha mazuri,"alisema.

Alipoulizwa iwapo haoni umri na elimu vinaweza kuwa kikwazo kwake kuwania ubunge, Majuto alisema umri si tatizo kwa sababu wapo wabunge wenye umri mkubwa kuliko wa kwake.

Mkongwe huyo alisema pia kuwa, elimu si tatizo kwa sababu elimu aliyonayo inamruhusu kuwania nafasi hiyo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na CCM. Majuto ni muhitimu wa elimu ya msingi.

“Kuna watu wanaweza kusema labda njaa ndio inayonifanya niingie kwenye siasa na kutaka kuwania nafasi kubwa ya ubunge, lakini lazima wajue kuwa sina njaa kwa kuwa kazi ninayoifanya inanipatia fedha za kutosha na maisha yangu ni mazuri,"alisema msanii huyo.

“Nina mpangilio mzuri wa kazi zangu, bado naheshimika kwa kiasi kikubwa na kazi zangu zinapendwa, ila kuingia kwenye siasa ni kwa sababu nina malengo mazuri na wanananchi wa Tanga Mjini na Tanzania kwa ujumla, hivyo hakuna wa kunizuia,” alisisitiza Majuto.

Majuto alisema hana hofu na majina ya wanasiasa maarufu, atakaopambana nao katika harakati zake hizo, kuanzia ndani ya CCM na kutoka vyama vya upinzani.

Iwapo Majuto atatekeleza mkakati wake huo kwa vitendo, atakuwa amefuata nyayo za baadhi ya wasanii waliojitosa kwenye ulingo wa siasa na kupata ubunge. Miongoni mwa wasanii hao ni Joseph Mbilinyi 'Sugu', mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Kepteni John Komba, mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya CCM.

Majuto ni miongoni mwa wasanii wenye mashabiki wengi nchini kutokana na umahiri wake wa kucheza filamu za vichekesho na za kawaida. Ni msanii aliyetokea mbali katika fani hiyo, ikilinganishwa na wasanii wengi waliopo sasa.

King Majuto amekuwa mwigizaji wa vichekesho kwa miaka 55 sasa, akijivunia mafanikio makubwa na kutambuliwa hata kimataifa.
Alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka 10. Wakati huo alikuwa darasa la pili katika shule ya msingi ya Msembweni mjini Tanga.

Baada ya kumaliza darasa la saba 1966, alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kudumu nalo hadi 1970, alipoamua kuachana nalo kutokana na kukosa nafasi ya kufanya sanaa kama ndoto zake zilivyokuwa zikimwelekeza. 
     
Kabla ya kujitosa kwenye sanaa, Majuto aliwahi kufanyakazi katika kikosi cha Zimamoto, Kiwanda cha Mablanketi na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), akiwa mlinzi.

Majuto alianza sanaa kwa kuigiza sauti za makabila mbalimbali. Alitengeneza kanda za kaseti za sauti yake na kuziuza, ambapo anakiri kwamba alipata pesa nyingi.

Kikundi chake cha kwanza kilikuwa DDC Kibisa, alichojiunga nacho 1982. Ni katika kikundi hicho, ndipo akapachikwa jina la King Majuto kwa maana ya Mfalme wa Kulia. Maigizo yake mengi yalikuwa ya kuhuzunisha na kuwatoa machozi mashabiki.

Hata hivyo, Majuto alianza kunufaika na kazi zake baada ya kuanzishwa kwa vituo vya televisheni nchini, ambapo alipata nafasi ya kucheza filamu za vichekesho na kulipwa fedha nyingi.

Kwa sasa, Majuto anamiliki nyumba kadhaa pamoja na magari ya biashara mjini Tanga. Ni msanii pekee wa vichekesho, anayelipwa fedha nyingi kuliko wasanii wengine wa fani hiyo.

No comments:

Post a Comment