KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 3, 2013

NORA AWEKA REHANI SIMU YA MKONONI



MSANII nyota wa filamu nchini, Nuru Nassor 'Nora' ameweka dhamana ya simu yake aina ya Samsung Galaxy ili kufidia deni analodaiwa katika nyumba ya kulala wageni ya Samaria iliyopo Ubungo Makuburi, Dar es Salaam.

Mbali na dhamana hiyo, msanii huyo alilipa sh. 90,000 kwa uongozi wa nyumba hiyo ya wageni ili kufidia deni alilokuwa akidaiwa.

Mkuu wa kituo kidogo cha Polisi cha Mwongozo kilichopo Ubungo Extrenal, Meja Haule, alisema jana kuwa, Nora ameweka dhamana ya simu pamoja na kiasi hicho cha fedha ili kupunguza deni la sh. 250,000 analodaiwa.

Haule alisema uongozi wa nyumba hiyo ya kulala wageni pamoja na Nora walifikia makubaliano ya kulipa deni hilo kwa maandishi baada ya gari la msanii huyo kushikiliwa kituoni hapo hadi atakapolipa deni hilo.

Alisema msanii huyo aliahidi kumalizia deni la sh. 65,000 zilizobaki jana jioni, lakini hadi gazeti hili lilipokuwa linakwenda mtamboni, alikuwa bado hajalipa fedha hizo na kukomboa simu pamoja na gari lake.

"Juzi baada ya kuhangaika huku na kule, alilipa sh. 90,000, akaweka na simu kama dhamana, hivyo akimaliza deni atapatiwa gari lake," alisema Haule.

Juzi, Nora alifikishwa katika kituo kidogo cha Polisi cha Mwongozo akidaiwa sh. 250,000 baada ya kushindwa kulipa fedha hizo kutokana na huduma za malazi alizopatiwa katika nyumba hiyo ya wageni kwa siku saba.

Nora alipanga katika nyumba hiyo akidai kuwa, anafanya kazi ya kuandaa filamu yake mpya, hivyo angelipa deni hilo baada ya kumaliza kazi yake.

Lakini baada ya kukamilisha kazi yake, alikataa kulipa deni hilo na kusema kuwa hana fedha hadi atakapoletewa na bosi wake. Hata hivyo, bosi wake hakutokea.

Baada ya kutokea hali hiyo, uongozi wa nyumba hiyo ya wageni ulizuia gari lake aina ya Vitz lenye namba za usajili T637 BZU, ambapo Nora alikimbilia Polisi kutaka wamsaidie aweze kupewa gari lake.

Tukio hilo ni la pili kwa msanii huyo. Siku tatu zilizopita, alifikishwa kituoni hapo kwa kosa la kupigana baada ya kushindwa kulipa deni la sh. 3,000 katika hoteli ya Lunch Time iliyopo Ubungo External, Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, Nora alifungua jalada la kesi ya shambulio la kudhuru mwili lenye namba MWP RB 1171/2013 baada ya kujeruhiwa na mhudumu wa hotel hiyo kutokana na kushindwa kulipa fedha hizo. Jalada la kesi hiyo limehamishiwa katika kituo cha Polisi cha Mbezi, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment