KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 24, 2013

KIM POULSEN KUIUNDA UPYA KILIMANJARO STARS


KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameahidi kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha Tanzania Bara, kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji, itakayofanyika mwezi ujao nchini Kenya.

Kim alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, mabadiliko hayo yamelenga kuiwezesha timu hiyo kutwaa kombe hilo baada ya kulikosa kwa miaka mitatu.
 
Kocha huyo kutoka Denmark alisema, anataka kutengeneza kikosi imara na chenye wachezaji wengi chipukizi, aliowaona wakati wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Kim alisema anatarajia kutangaza kikosi kitakachoshiriki michuano hiyo wakati wowote ili kiweze kuingia kambini mapema kwa ajili ya kujiandaa na michuano hiyo.

Michuano ya Kombe la Chalenji, inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), itafanyika Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.

Nchi wanachama wa CECAFA, zilizothibitisha kushiriki katika michuano hiyo ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania Bara, Uganda na Zanzibar.

Michuano hiyo itatanguliwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA, utakaofanyika Novemba 26 mwaka huu, ambao pamoja na mambo mengine, utakuwa na ajenda ya uchaguzi. Uchaguzi huo ni kwa ajili ya kujaza nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wajumbe wanaomaliza muda wao ni Sahilu Gebremarian wa Ethiopia, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CECAFA, Abdigaani Saed Arab (Somalia), Tariq Atta (Sudan) na Raoul Gisanura (Rwanda).

No comments:

Post a Comment