KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 8, 2013

KAMATI YA JAJI LUANDA KUSIKILIZA RUFANI ALHAMISI



Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda itakutana keshokutwa (Oktoba 10 mwaka huu) kusikiliza rufani zilizowasilishwa mbele yake.

Waombaji uongozi watatu wamekata rufani katika Kamati ya Jaji Luanda wakipinga kutopitishwa kugombea katika uchaguzi wa TFF, uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ajili ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Warufani ni Samwel Nyalla aliyeondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda namba 2 ya mikoa ya Mara na Mwanza kwa kutojaza kikamilifu fomu namba 1 ya maombi ya kugombea uongozi TFF kwa kutoonesha malengo yake.

Ayoub Nyaulingo yeye anapinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda namba 6 (Katavi na Rukwa) kwa kutokuwa na uzoefu uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.

Naye Ayoub Nyenzi amekata rufani kupinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha Kanda namba 7 (Iringa na Mbeya) kwa kushindwa kuthibitisha uraia wake.

UCHAGUZI BODI YA LIGI SASA OKTOBA 25

Uchaguzi wa viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) sasa utafanyika Oktoba 25 mwaka huu badala ya Oktoba 18 mwaka huu.

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesogeza mbele uchaguzi huo kutokana na maombi ya Kamati ya Ligi kwa vile baadhi ya wajumbe wa Baraza la Bodi hiyo kuwa vilevile wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

TFF itafanya Mkutano Mkuu wake Oktoba 26 mwaka huu ambao utakuwa na ajenda za kawaida kama zilivyoainishwa katika Katiba yake wakati ajenda ya uchaguzi itakuwa Oktoba 27 mwaka huu.

Wagombea uongozi TPL Board ni Hamad Yahya Juma anayewania nafasi ya Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Said Muhammad Abeid. Wanaowania nafasi za ujumbe katika Kamati ya Uongozi ni Kazimoto Miraji Muzo na Omar Khatib Mwindadi.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbwezeleni inatarajia wakati wowote kutangaza tarehe ya kuanza kampeni kwa wagombea katika uchaguzi huo. Baraza la Bodi linaundwa na wajumbe 38 ambao ni wenyeviti 14 wa klabu za Ligi Kuu na wenyeviti 24 wa klabu za Daraja la Kwanza.

No comments:

Post a Comment