'
Tuesday, October 1, 2013
FIFA YAIVUTIA PUMZI YANGA, MADAI YA PAPIC YAANZA KUJADILIWA
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limewasilisha rasmi suala la madai ya aliyekuwa Kocha wa Yanga, Kostadin Papic dhidi ya klabu hiyo katika Kamati ya Hadhi ya Wachezaji.
FIFA imesema imepeleka rasmi suala hilo katika kamati yake hiyo baada ya kupokea vielelezo vya Papic anayedai kuidai Yanga dola 10,000 za Marekani pamoja na vile vya Yanga inayodai kumlipa kocha huyo fedha zote alizokuwa akiidai klabu hiyo.
Kwa taratibu za FIFA, hivi sasa haitapokea vielelezo vingine kutoka pande hizo mbili, na badala yake Kamati hiyo inayoongozwa na Theo Zwanziger kutoka Ujerumani itafanya uamuzi na kuziarifu pande husika. Zwanziger kitaaluma ni mwanasheria.
Papic aliyeinoa Yanga kwa vipindi viwili tofauti aliwasilisha malalamiko yake FIFA akidai hadi mkataba wake unamalizika klabu hiyo ilikuwa haijamlipa dola 10,000 za Marekani.
LIPULI, MAJIMAJI KUUMANA WAMBI FDL
Mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Lipuli ya Iringa na Majimaji ya Songea sasa itachezwa kesho (Oktoba 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Wambi uliopo Mafinga badala ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora kwa ajili ya shughuli za mbio za Mwenge.
Mechi nyingine ya FDL kesho itakuwa kati ya Tessema FC ya Dar es Salaam na Ndanda FC ya Mtwara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment