KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 20, 2013

ILOMBE MBOYO, MWANASOKA ALIYEIBULIWA AKIWA JELA


BRUSSELS, Ubelgiji
MAISHA ya binadamu yanapitia katika njia nyingi. Wakati mwingine binadamu anaweza kukumbana na vikwazo vingi na vya kila aina, vinavyoweza kumkatisha tamaa ya maisha, akamua kuachana na kile alichokuwa akikitafuta.

Lakini wakati mwingine, vikwazo hivyo huweza kumsukuma binadamu akabiliane vyema na changamoto iliyoko mbele yake ili akipate anachokitaka. Hiyo ni mifano michache, inayoweza kutumika kumuelezea mwanasoka Ilombe Mboyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliyechukua uraia wa Ubelgiji.

Ilombe alizaliwa Congo na kukulia katika mji wa Brussels  nchini Ubelgiji, ambako alikuwa na mazoea ya kucheza soka kwenye bustani za mji huo. Baadhi ya vijana aliozoea kucheza nao soka kwenye maeneo hayo ni pamoja na Vincent Kompany, ambaye kwa sasa ni nahodha wa Manchester City na Ubelgiji.

Mwanasoka huyo alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela mwaka 2004, akiwa na umri wa miaka 17, baada ya yeye na vijana wenzake kupatikana na hatia ya kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 14. Alikuwa mmoja wa vijana watukutuku katika kitongoji cha Matonge kilichoko katika mji wa Brussels.

Ilombe ni mmoja wa wachezaji waliokuwa wakiwindwa kwa udi na uvumba na klabu ya West Ham ya England, lakini usajili wake uliota mbawa baada ya mashabiki wa klabu hiyo kufichua kuhusu kesi yake ya ubakaji kupitia mtandao wa twitter.

Mashabiki hao waliona kuwa, lisingekuwa jambo zuri kwa mtu aliyehukumiwa kifungo jela kwa kosa la ubakaji, kupata umaarufu na utajiri kupitia soka ya kulipwa. Waliitaka klabu yao ifute mipango ya kumsajili.

Lakini mchezo wa soka ulifanikiwa kubadili tabia na mwenendo wa Ilombe, ambaye amekiri kuwa, jela iliyabadili maisha yake.

"Nilipokuwa jela, kwa mara ya kwanza, niliweza kubaini uzito wa kile nilichokifanya,"alisema Ilombe alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) hivi karibuni.

"Niliamua kubeba jukumu la kujirekebisha," alisimulia mshambuliaji huyo mwenye kipaji cha hali ya juu cha kusakata kabumbu.

Pierre Bodenghien (58) ndiye aliyevumbua kipaji cha Ilombe wakati alipokuwa akitumikia adhabu yake kwenye gereza la Ittre.

"Alikuwa na kila kitu kinachohitajika kwa mwanasoka, kuanzia umbo, mbinu na nguvu za mwili,"anakumbuka Pierre. "Alikuwa na uwezo wa kutumia miguu yote miwili."

Pierre alimshuhudia Ilombe akicheza soka wakati wa kipindi cha mazoezi ya mchezo huo kwenye jela ya Ittre. Utaratibu wa kuwaruhusu wafungwa kucheza soka ulianzishwa mwaka 1995 na Princess Paola (sasa Malkia Paola) wa Ubelgiji

Akiwa mvumbuzi wa vipaji vya soka kwa miaka zaidi ya 20, Pierre aliweza kubaini kipaji cha Ilombe baada ya kumuona akicheza mchezo huo kwenye jela ya Ittre na kuwapa taarifa waajiri wake, klabu ya Charleroi.

Kutokana na Ilombe kuonyesha tabia nzuri wakati akiwa jela, mipango ikaanza kufanywa kupitia bodi za Parole ili kumruhusu mchezaji huyo kufanya mazoezi na klabu hiyo.

Charleroi ilikuwa ikiongozwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Scotland, John Collins, ambaye anakumbuka vizuri wakati Ilombe alipoanza kufanya mazoezi na timu hiyo.

"Alikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kutoa pasi. Baadaye tulianza kumualika kwenye mechi za majaribio," anasema Collins.

Kwa mujibu wa Collins, licha ya kuruhusiwa kufanya mazoezi kwenye klabu hiyo, Ilombe alikuwa akilazimika kurudi jela mara moja au mbili kwa wiki.

"Alikuwa mpole, kama unavyoweza kutarajia kwa mtu aliyetoka jela na kujiunga na klabu ya kulipwa. Alikuwa mchezaji mwenye nguvu na mbinu za hali ya juu za kisoka," anasema Collins.

"Tabia yake ilikuwa nzuri. Ilikuwa ikipendeza kumuona akibadilika kitabia na kushirikiana vyema na wenzake. Kila mmoja anastahili kupewa nafasi kwa mara ya pili,"anasisitiza Collins.

Baada ya kulivutia benchi la ufundi wakati wa mechi za majaribio, Ilombe alisajiliwa na Charleroi mwaka 2009, lakini usajili huo ulifutwa na mahakama ya Ubelgiji.

Ilombe alisajiliwa na klabu ya Kortrijk ya Ubelgiji kwa mkataba wa kudumu Septemba 2010 na miezi minne baadaye, alijiunga na klabu ya Gent, ambako alionyesha kipaji cha hali ya juu cha kucheza soka baada ya kuifungia mabao 37 katika mechi 80. Ni katika klabu hiyo alipachikwa jina la utani la 'Le Petit Pele'. Baadaye alipewa unahodha.

Mwanasoka huyo alisajiliwa na Genk Agosti mwaka huu kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 3.5 baada ya mipango yake ya kujiunga na West Ham kukwama.

Ilombe ameichezea Ubelgiji mechi mbili za kimataifa wakati wa michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika Brazil. Chipukizi huyo huenda akacheza pamoja na nyota wengine wa Ubelgiji katika fainali hizo kama vile Christian Benteke, Marouane Fellaini, Dries Mertens, Eden Hazard na Kompany.

Chama cha Soka cha Ubelgiji kilimuunga mkono mchezaji huyo alipoitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo mwaka jana. Rais wa chama hicho, Francois De Keersmaeker alisema: "Mtu anapomaliza kutumikia adhabu ya kifungo, hapaswi kutoweka katika jamii. Mboyo (Ilombe) anaweza kuwa mfano wa vijana wanaopotea njia."

West Ham ilionyesha dhamira ya kumsajili Ilombe mwanzoni mwa msimu huu kabla ya mashabiki wa klabu hiyo kugundua kuhusu kifungo alichowahi kukitumikia na kuendesha kampeni ya kuzuia usajili wake kupitia twitter.

Mmiliki wa West Ham, David Sullivan aliamua kufuta mpango wa kumsajili mchezaji huyo na kusema: " Sikuweza kwenda kinyume na mashabiki. Tunataka maoni yao na wameonekana kusema hapana."

Badala yake, Ilombe alilazimika kujiunga na Genk, moja ya klabu kubwa za Ubelgiji kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 3.5.

Ilombe amepata mafanikio makubwa msimu huu baada ya kuifungia Genk mabao saba katika michuano ya ligi ya Ubelgiji na ile ya Ulaya.

Pierre, ambaye alivumbua kipaji cha Ilombe wakati akiwa jela, ameeleza kuvutiwa na mpango wa serikali ya nchi hiyo wa kuanzisha programu maalumu ya kuwaruhusu wafungwa kucheza mchezo huo.

"Mara mbili kwa wiki, wafungwa 30 wanaruhusiwa kufanya mazoezi nje ya jela na wengi zaidi wanataka kushiriki,"anasema Pierre. "Ni mpango mzuri, unahusisha vifaa bora na makocha."
Kwa mujibu wa Ilombe, mpango huo umewawezesha wafungwa kujifunza mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuwa na nidhamu na jinsi ya kuwa sehemu ya timu.

"Wakionyesha utovu wa nidhamu jela, hupewa adhabu ya kutoruhusiwa kwenda kufanya mazoezi uraiani,"anasema Collins.

Mmoja wa wanasoka nyota wa zamani wa Ubelgiji, Enzo Scifo ni miongoni mwa watu wanaohusika na programu hiyo.

Enzo amekuwa akizungumza na wafungwa, ambao wengi walikuwa wakivutiwa na kipaji chake alipokuwa akicheza soka. Awali, Enzo alionyesha woga wa kufanyakazi hiyo, kutokana na mazingira yalivyokuwa, lakini baadaye alizoea.

Hali ya usalama gerezani wakati wa mazoezi ya soka ni kubwa na Pierre na makocha wenzake hupata ulinzi mkali. Wakati wafungwa wanapocheza soka, hawapigani wala kujihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya.
 
"Katika kipindi cha miaka 18 iliyopita, nimeshuhudia wafungwa wakipigana mara moja. Wamekuwa wakicheza mechi za wachezaji watano kila timu na ile inayoshinda, inaendelea na mchezo hadi itakapofungwa,"anasema Pierre.

Programu hiyo, iliyoanzishwa kwenye gereza la Ittre kwa sasa imesambazwa kwenye magereza mengine 12 nchini humo

Ilombe alizaliwa Aprili 1987 katika mji wa Kinshasa nchini Congo. Klabu alizochezea ni
Charleroi (2009-10), Kortrijk (2010-11) na Gent (2011-13). Ameichezea Ubelgiji mechi mbili za kimataifa.

No comments:

Post a Comment