KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 31, 2013

BLATTER, HAYATOU WAMPONGEZA MALINZI


Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Jamal Malinzi ameendelea kupokea salamu za pongezi baada ya kushinda wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Salamu nyingine za zimetoka kwa Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter ambapo amempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake ya kuongoza mchezo huo nchini.

Blatter amesema ana uhakika ufahamu wake na uwezo wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini, na kuongeza kuwa milango ya FIFA iko wazi wakati wowote anapotaka kujadili masuala yanayohusu mchezo huo.

“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele yenu,” amesema Rais Blatter katika salamu zake.

Wengine waliomtumia Rais Malinzi salamu za pongezi ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, Rais wa Heshima wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Arumeru (ADFA), Peter Temu.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Katika salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira wa miguu Afrika, Rais Hayatou amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.

Amesema CAF ina imani uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika mpira wa miguu havitausaidia mpira wa miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha zaidi vijana wa bara hili.

Rais Hayatou amemtakia Rais Malinzi kila la kheri katika kipindi chake cha uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko pamoja naye katika kusukuma mbele gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.

No comments:

Post a Comment