KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 28, 2013

DAUDI SALUM 'BRUCE LEE': VIONGOZI WA SOKA BONGO WABABAISHAJI



Asema wanawania uongozi ili kufanya biashara
Ajivunia rekodi zake tatu za kimataifa

KWA mashabiki wa soka wanaolikumbuka jina la Daudi Salum, bila shaka wataikumbuka vyema staili yake ya uchezaji, iliyomfanya apachikwe jina la Bruce Lee.

Alikuwa beki kisiki, mwenye kasi na asiyepitika kirahisi. Na kila alipokuwa akiondosha mpira kwenye eneo lake la hatari, alipenda kuruka kwa staili ya kungfu. Hiyo ndiyo sababu iliyowafanya mashabiki wampachike jina la Bruce Lee.

Sababu nyingine iliyowafanya mashabiki wampachike jina hilo ni rangi yake. Alikuwa na weupe uliong'ara na kufanya iwe rahisi kumtambua mara moja awapo uwanjani. Ilikuwa rangi adimu kwa wachezaji wakati huo.

Pamoja na umri mkubwa alionao sasa, rangi ya Daudi bado ni ile ile. Tofauti ipo kidogo kwenye umbo na hii ni kutokana na umri. Lakini bado ana ukakamavu. Pengine kutokana na majukumu ya kazi yake.

Daudi alikuwa mmoja wa wanasoka wa timu ya Taifa, Taifa Stars iliyofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za 1980 zilizofanyika nchini Nigeria na kutolewa hatua ya makundi baada ya kufungwa mechi mbili na kutoka sare moja.

Beki huyo mkongwe pia alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichotolewa na Mehala El-Kubra ya Misri katika nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika 1974.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Simba iliichapa Mehala El-Kubra bao 1-0 na ziliporudiana mjini Cairo, ilichapwa idadi hiyo ya bao. Mshindi ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano.

Daudi pia alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichoonyesha maajabu katika michuano hiyo mwaka 1975, ambapo baadaya kuchapwa mabao 4-0 na Mufurira Wanderers ya Zambia mjini Dar es Salaam, kikashinda mabao 5-0 katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini Lusaka, Zambia.

Hizo ndizo rekodi za kujivunia alizonazo sasa mwanasoka huyo mkongwe na ambazo anasema ni nadra kwa wachezaji wa sasa kuweza kuzifikia.

"Tatizo la wachezaji wa sasa ni kwamba wanakosa ari ya kufikia mafanikio ya aina hii,"alisema Daudi alipozungumza na mwandishi wa makala hii kwa njia ya simu baada ya juhudi za kukutana naye ana kwa ana kushindwa kufanikiwa.

Nililazimika kuzungumza na Daudi kwa njia ya simu kwa sababu kumpata na kuzungumza naye ana kwa ana ni kazi ngumu. Hii ni kutokana na majukumu yake kikazi. Muda mwingi yupo bize.

Tofauti na wanasoka wengine wa zamani, kwa sasa Daudi havutiwi sana na mchezo huo. Inawezekana ni kwa sababu ya majukumu yake kikazi, lakini pia kutofurahishwa na mwenendo wa mchezo huo hivi sasa.

"Mchezo wa soka hivi sasa umegeuzwa kuwa biashara. Viongozi wa sasa wameshindwa kuweka mbele zaidi. Wameugeuza mchezo huo kuwa biashara,"alisema Daudi.

"Watu wameamua kuingia kwenye soka kwa sababu ya kufanya biashara. Hawana malengo ya dhati ya kuendeleza mchezo huo kama ilivyokuwa kwa viongozi wa zamani,"aliongeza.

Kwa mujibu wa Daudi, hali hii ndiyo iliyosababisha viongozi wengi wa soka nchini kuonekana kuwa wababaishaji kwa vile wamelenga kujinufaisha zaidi wao binafsi.

Daudi alisema enzi zao, wanasoka wengi walikuwa wakicheza mchezo huo kutokana na mapenzi waliyokuwa nayo kwa klabu zao na kwamba waliweza mbele zaidi uzalendo kwa nchi yao.

Alisema pia kuwa, nidhamu kwa wachezaji wa zamani ilikuwa juu na kwamba haikuwa rahisi kwa mchezaji kuonyesha utovu wa nidhamu kwa viongozi au ndani na nje ya uwanja.

Mkongwe huyo alisema enzi zao hakukuwa na malipo makubwa ya pesa kwa wachezaji kama ilivyo sasa, lakini walicheza kwa ari kubwa na kujituma kwa sababu ya mapenzi waliyokuwa nayo kwa mchezo huo.

"Enzi zetu, timu ya taifa ilikuwa ikipata huduma nzuri. Tuliwekwa kambini kwenye hoteli kubwa kama vile Bahari Beach au Kunduchi Beach na tulipata huduma zote muhimu. Ilikuwa vigumu kwa mchezaji kwenda nje ya misingi ya kambi,"alisema beki huyo mkongwe.

"Lakini wachezaji wa sasa wana matatizo na wengi hawana nidhamu ndio sababu wanashindwa kucheza soka kwa muda mrefu na kuziletea timu zao mafanikio," aliongeza.

Mwanasoka huyo mkongwe alisema ni makosa kuilaumu serikali kwa kushindwa kuendeleza michezo nchini wakati vyama vya michezo havionyeshi juhudi zozote katika kuiendeleza .

Alisema viongozi wa vyama vya michezo wanapaswa kuonyesha juhudi binafsi katika kuendeleza michezo wanayoiongoza ndipo serikali inapoweza kuingiza mkono wake.

"Hakuna mtu anayeweza kuwekeza kwenye tope. Unawekeza mahali penye neema. Panapokuwepo viashiria vizuri ndipo mwekezaji anaposhawishika kuwekeza,"alisisitiza mwanasoka huyo.

"Kwa hiyo hatuwezi kuilaumu serikali wakati ambapo viongozi wenyewe ni wabinafsi na wameweka mbele zaidi maslahi yao binafsi,"alisisitiza.

Daudi pia ameuponda utaratibu unaotumiwa sasa na baadhi ya klabu kubwa za soka nchini kupapatikia kusajili wanasoka wengi wa kigeni wakati uwezo wao ni mdogo. Alisema kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa wanasoka wazawa.

Alisema klabu inaposajili wachezaji wengi wa kigeni, inawavunja nguvu wazawa, ambao baadhi yao kiwango cha ni cha juu, lakini hawathaminiwi.

"Huwezi kuleta mchezaji wa kigeni, ambaye kiwango chake ni kibovu ukategemea kupata maendeleo. Hayo ni matumizi mabaya ya fedha za klabu na yanaonyesha ni mbinu za kuhalalisha ulaji,"alisema.

Daudi ametoa mwito kwa serikali kuendeleza mashindano ya shule za msingi na sekondari, ambayo alisema miaka ya nyuma ilikuwa chimbuko la wanasoka wengi waliochezea klabu za Simba, Yanga na Taifa Stars.

No comments:

Post a Comment