KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

KASEJA MBAYAAAA!



KIPA namba moja wa klabu ya Simba na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Juma Kaseja ameelezwa kuwa kikwazo kikubwa kwa makipa wenzake kupata namba kwenye timu hizo.

Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, makipa wote waliowahi kusajiliwa na Kaseja katika kikosi cha Simba ilikuwa nadra kwao kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kuna baadhi ya misimu, Kaseja aliidakia Simba mechi zote za ligi kuu ya Tanzania Bara na kuwaacha makipa wenzake wakisugua benchi.

Uchunguzi huo umabaini kuwa, sababu kubwa inayomfanya Kaseja apate namba ya kudumu Simba ni uwezo wake wa kulinda lango, kuwapanga mabeki na kucheza kwa kujituma.

Baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakimuhusi Kaseja kwamba anatumia ndumba kuwamaliza makipa wenzake, lakini imebainika kuwa tuhuma hizo hazina msingi.

Kaseja ndiye kipa mkongwe kuliko wote waliopo nchini hivi sasa na amekuwa akitunza kiwango chake kutokana na kufanya mazoezi kwa bidii na kutojihusisha na mambo ya anasa.

Baadhi ya makipa waliowahi kusugua benchi Simba wakiwa na Kaseja ni pamoja na Ally Mustapga 'Barthez', Kevin Mhagama, Shaaban Kado, Hamad Waziri, Wilbert Mweta na Deogratius Munishi.

Kati ya makipa hao, Bathez ndiye pekee aliyebahatika kucheza katika baadhi ya mechi muhimu na pia kuwa kipa namba moja wa Simba wakati Kaseja alipojiunga na Yanga msimu wa 2008/2009.

Waziri, ambaye alisajiliwa na Simba kwa mbwembwe msimu huu akitokea JKT Oljoro ya Arusha aliamua kufungasha virago baada ya kuonyesha kiwango cha chini kama ilivyokuwa kwa Mweta.

Hali hiyo pia imekuwa ikijitokeza kwenye kikosi cha Taifa Stars, ambapo Kaseja amekuwa akiwafunika makipa wenzake na kuwa chaguo la kwanza kwa makocha wa timu hiyo.

Kipa pekee, aliyekuwa akimpoka namba Kaseja kwenye kikosi hicho alikuwa Ivo Mapunda, ambaye alikuwa chaguo namba moja la kocha wa zamani wa timu hiyo, Marcio Maximo.

Kwa sasa, Simba imemsajili kipa wa kimataifa wa Uganda, Abbel Dhaira, ambaye alikuwa akicheza soka ya kulipwa Iceland, lakini upo uwezekano mkubwa naye akasugua benchi.

Tangu aliposajiliwa na Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo, Dhaira hajapata nafasi ya kuichezea timu hiyo katika mechi za ligi kuu.

Mganda huyo alikuwa kipa wa akiba wakati Simba ilipocheza na Libolo ya Angola katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa umbo na urefu, Dhaira anaweza kuonekana kipa bora kuliko Kaseja, hasa kwa makocha wa Ulaya, lakini kutokana na umahiri wa Mtanzania huyo, anaweza kujikuta akisugua benchi msimu mzima na kulipwa mshahara wa bure.

No comments:

Post a Comment