KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 7, 2013

KABANGE TWITE APEWA ULAJI YANGA



LICHA ya usajili wa beki, Kabange Twite kushindikana katika dirisha dogo la usajili, ambalo lilifungwa mwezi uliopita, beki huyo ataendelea kufaidi mshahara na posho za Yanga mpaka mwisho wa msimu huu.

Akizungumza na waandishi wa habari za michezo kwenye Hoteli ya JB Belmont iliyopo katika jengo la Quality Centre mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji alisema wataendelea kumtunza mchezaji huyo kwa ajili ya kumtumia msimu ujao.

Alikiri kulitokea makosa katika mchakato wa usajili wa Kabange na kutokana na umuhimu walionao kwake, atabaki katika klabu hiyo mpaka mwisho wa msimu.

"Kulitokea makosa kidogo katika suala lake la usajili, lakini tumeamua atabaki Yanga na atakuwa analipwa mshahara wake kama kawaida," alisema Manji.

Klabu hiyo pia imekiri kuwa, kipa Yaw Berko anaidai Yanga na anatarajiwa kulipwa kabla ya kumalizika wiki hii.

Manji, ambaye alikataa kutaja kiasi cha fedha, anazodai nyanda huyo raia wa Ghana, alisema kabla ya kufika Jumapili, watamlipa chake ili aondoke nchini.

Berko alishindwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kudakia timu ya FC Lupopo licha ya kufuzu majaribio kutokana na kudai Yanga fedha zake. Manji alisema Berko atalipwa na kuruhusiwa aende kujiunga na klabu hiyo.

Mwenyekiti huyo wa Yanga, ambaye alitumia mkutano huo kufafanua masuala mbalimbali ya klabu hiyo, alisema mjumbe wa kamati ya utendaji aliyesimamishwa, Tito Osoro hajafukuzwa kama inavyodhaniwa.

Alisema amesimamishwa ili kutazamwa mwenendo wa tabia yake kama amejirekebisha au la.

Manji amewataka wanachama wa Yanga kuacha tabia ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari kuzungumza masuala ya klabu, badala yake watumie vikao na mikutano.

No comments:

Post a Comment