'
Sunday, February 17, 2013
UCHAGUZI MKUU TFF WAPIGWA STOP
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesimamisha uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Lyatto alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, sababu za kusimamishwa kwa uchaguzi huo ni kukiukwa kwa baadhi ya kanuni.
Lyatto alisema kamati yake itatangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo baada ya kurekebishwa kwa kasoro hizo, ambazo alidai kuwa kwa sasa ni siri.
Alisema kamati ya uchaguzi itashughulikia haraka tatizo hilo kabla ya kutangazwa kwa tarehe nyingine ya uchaguzi huo.
Mwenyekiti huyo alisema uamuzi wa kusimamisha uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa mamlaka ya kamati ya uchaguzi kupitia ibara ya 10 (5).
"Ndugu zangu natangaza kusimamisha uchaguzi hadi hapo matatizo yaliyopo katika kanuni yatakapowekwa sawa, lakini kwa sasa kanuni zilizoleta matatizo ni siri,"alisema.
Uchaguzi mkuu wa TFF uliingia mizengwe baada ya Kamati ya Rufani ya TFF kuwaengua Jamal Malinzi na Yahya Ahmed kugombea nafasi ya rais wa shirikisho hilo na mwenyekiti wa bodi ya ligi kwa madai ya kukosa sifa.
Kamati hiyo inayoongozwa na Iddi Mtiginjola, ilimuengua Malinzi kwa kutumia kifungi cha 9 (3) kwa madai kuwa, hana uzoefu wa uongozi wa miaka mitano na uadilifu.
Mgombea mwingine aliyeenguliwa ni Michael Wambura kwa kigezo cha kutokuwa muadilifu, alipokuwa katibu mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT).
Kuenguliwa kwa wagombea hao kulizusha malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa soka nchini, ambao walihoji iweje Malinzi aonekane hana sifa wakati alipitishwa kuwania wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa 2008.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwataka wagombea walioenguliwa, kuiomba kamati ya rufani ipitie upya uamuzi wake au kuwasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) au Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ya Michezo (CAS).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment