KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 4, 2013

KAPOMBE AILIZA SIMBA



SIMBA jana ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na JKT Ruvu katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Mabingwa hao watetezi itabidi wajilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani walifanikiwa kupata adhabu ya penalti dakika ya 87, lakini ilipotezwa na Shomari Kapombe.

Mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza aliamuru ipigwe penalti kwenda kwenye lango la JKT Ruvu baada ya beki Damas Makwaya kudaiwa alimwangusha Haruna Moshi ndani ya eneo la hatari.

Hata hivyo, shuti la Kapombe lilipanguliwa na kipa Shabani Dihile wa JKT Ruvu na mpira kugonga mwamba wa goli na uliporudi uwanjani, uliokolewa na mabeki wa timu hiyo.

Matokeo hayo yameifanya Simba iendelee kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 15. Yanga bado inaongoza kwa kuwa na pointi 33, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 30.

JKT Ruvu ililianza pambano hilo kwa kasi na kufanya shambulizi kali kwenye lango la Simba dakika ya saba wakati Kisimba Luambano alipoingia na mpira ndani ya eneo la hatari na kutoa pasi kwa Mussa Hassan, lakini shuti lake lilitoka nje.

Simba ilihesabu bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Amri Kiemba baada ya kipa Shabani Dihile kutema shuti la Abdalla Seseme na mpira kumkuta mfungaji, aliyeukwamisha wavuni.

Pambano hilo liliingia doa dakika ya 20 baada ya wachezaji wa JKT Ruvu kuanza kucheza rafu na kusababisha mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza kumuonyesha kadi ya njano Jimmy Shoji kwa kosa la kumuumiza Kiemba. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa JKT Ruvu kulishambulia lango la Simba mfululizo. Mashambulizi hayo yalizaa matunda dakika ya 63 wakati Nashon Matali alipofunga bao la kusawazisha kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mussa.

Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Paul Ngelema, Shomari Kapombe,Komabil Keita, Abdalla Seseme/Haruna Moshi, Haruna Chanongo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngasa/Abdalla Juma, Amri Kiemba, Ramadhani Chombo/Kigi Makassi.

JKT Ruvu: Shabani Dihile, Credo Mwaipopo/Mussa Holoa, Kessy Mapande, Kisimba Luambano, Damas Makwaya, Jimmy Shoji, Hussein Bunu, Nashon Matali, Mussa Hassan, Zahoro Pazi, Emmanuel Pius/Amos Juma.

No comments:

Post a Comment