KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 14, 2013

MADUDU HAYA YA TFF HAYAKUBALIKI



KWANZA niweke wazi mapema kwamba, siandiki hapa kwa ajili ya kumbeba mtu, hivyo sina maslahi binafsi bali maslahi kwa ajili ya mustakabali wa soka la Tanzania na Watanzania wenyewe.

Kuna tabia, ambayo imejengeka katika baadhi ya sekta nchini kujiona kwamba wao wako juu ya kila kichwa cha Mtanzania. Kujiona wao wanafikiri vyema zaidi kuliko Watanzania wengine na matokeo yake kutaka kulazimisha Watanzania wacheze ngoma wanazopiga wao.

Lakini pia tupo baadhi yetu, ambao huwa hatuangalii jina wala mkunjo wa sura ya mtu, anayetaka kutupigisha ngoma hizo, na badala yake hujazwa ujasiri kutoka roho wa bwana kuwakosoa, na kuwaonya kwa namna, ambayo tunaona inafaa.

Kwa msingi huo, ndiyo maana napenda nieleweke kabisa kwamba nimekuwa nikifuatilia mwenendo wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na kubaini bila shaka kwamba ni mtu anayeongoza kwa mtindo wa kujitoa.

Tenga anaongoza shirikisho hilo kwa mtindo wa kutaka kufurahisha watu na matokeo yake kufikia hatua ya kulifanya shirikisho hilo kuwa genge la wahuni kwa kufanya mambo ambayo sio ya kimichezo na kiutaratibu.

Hili limekuja kujidhihirisha katika sakata la uchaguzi linaloendelea sasa, ambapo kwa makusudi kabisa (nasisiti za makusudi, maana Tenga anajua undani wake), rais huyo ameamua kuiua TFF kwa ajili ya kuwafurahisha marafiki zake.

Kwani hata makosa ya wazi, ambayo yanahitaji busara tu kutatuliwa, anakaa kimya kana kwamba shirikisho hilo lipo kwa ajili ya genge la watu kufanyia shughuli zao.

Kwa mfano, leo watu wanahukumiwa kwa sababu eti waliukataa waraka uliosambazwa na shirikisho hilo na hivyo kuonekana kwamba hawana sifa ya kizalendo.

Hivi unapowapelekea waraka wanachama wapige kura juu ya kukubalika kwake au la, unategemea kupata majibu ya namna gani? Kwa nini TFF haikukaa na kufanya uamuzi wa kidikteta moja kwa moja kwa kuupitisha kuliko kuja kufanya udikteta ndani ya mfumo wa demokrasia waliouweka wenyewe?

Leo watu wazima na akili zao wanakaa na kumpitisha mtu mmoja kwamba ndiye aliye na sifa za kugombea urais, kana kwamba tupo kwenye mfumo wa kuchagua boksi na mtu.

Tenga na watu wake lazima wafahamu kwamba, TFF sio yao bali ya Watanzania, hivyo kutakiwa kuzingatia haki, kanuni na taratibu ili kuweka umoja na mshikamano wa kisoka kwa nchi nzima.

Kinachofanywa sasa ni kama kugeuza shirikisho hilo kuwa la kundi fulani la watu kufanikisha mambo yao na hivyo kutaka sura zingine, ambazo hazitokani na wao, zisionekane katika shirikisho hilo.

Wengine tunajua kwa undani urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani, Iddi Mtiginjola na Nyamlani, tena urafiki wa kufa na kuzikana na hatushangai kwa nini anamtengenezea mazingira ya kuwa mgombea pekee.

Hakuna asiyejua kwamba hayo yote yanafanyika katika mazingira ya hofu kwamba kama atapitishwa mgombea mwingine ashindane naye, basi uwezekano wa kuangushwa ni mkubwa.

Maana kuna vitu, ambavyo vinatia kichefuchefu kusikia kwamba Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, ambaye anagombea uenyekiti wa bodi ya ligi, eti anakuwa na sifa ya uzoefu katika soka kuliko alivyokuwa Yahya Mohamed.

Hata watu wasio na akili watajiuliza kati ya Yahya na Manji nani mwenye uzoefu katika soka? Yahya kaongoza Kagera Sugar kwa miaka mingi, Manji juzi tu kwenye Yanga, lakini leo anakuwa na sifa za kuwa mgombea pekee. Kama tunajiamini, kwa nini tunaogopa ushindani?

Pia, eti Nyamlani anakuwa na sifa ya uzoefu zaidi kuliko Jamal Malinzi, ambaye aliongoza Yanga kwa muda mrefu tu. Hivi unawezaje kumwaminisha Mtanzania kwamba uamuzi huu uko sahihi na asiache kufikiria mfumo wa kubebana?

Nampongeza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makalla kwa kuliona hilo na kuamua kusimamisha kampeni za wagombea kwa ajili ya uchaguzi huo. Yote aliyoyasema Makalla ni sahihi na sina sababu ya kuyarudia.

Ukweli unabaki palepale kwamba, Tenga na kundi lake lazima wajue kwamba, TFF ni yetu sote kwa maendeleo ya Watanzania, ambao ni wapenzi wakubwa wa mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati. Kuendelea kukumbatia mambo haya ya hovyo hakuna atakayeunga mkono.

Haitashangaza kabisa kwamba hata waraka uliopitishwa kwa kuweka vigezo mbalimbali, vikiwemo vya uzeofu, ulilenga kuwabana baadhi ya watu na kuwabeba watu wengine.

Hili limejitokeza wazi na hakuna shaka kwamba baada ya kufanikiwa kuingiza watu wao, haitashangaza tena kuona viongozi wateule hao wakabadilisha waraka huo ili kuendana na matakwa ya wengi.

Tenga alijijengea imani kwa baadhi ya Watanzania, lakini kumbe ana vichwa viwili ndani ya kuaminiwa huko na matokeo yake, kumaliza uongozi wake kwa staili ya ajabu. Tunasikia anajiandaa kwenda kuongoza Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lakini kwa staili hii, sijui kama ataweza kufanikiwa.

Kama unaamua kuunguza kwa makusudi nyumba yako na kukimbilia kwa jirani kuishi kwenye nyumba nzuri zaidi, unakuwa umetumia akili za namna gani? Nasema bila kumung’unya maneno, Tenga amemaliza uongozi wake kwa staili, ambayo haiwezi kuwafurahisha watanzania.

Huwezi kuacha mambo ya hovyo yafanyike mbele yako bila kuyakemea, ukidhani historia itakukumbuka na ndiyo maana soka letu linazidi kwenda kuzimu kwa sababu ya utaratibu huu wa hovyo.

Tabia ya kubebana sehemu yoyote inapokumbatiwa, matokeo yake ni kwamba yale malengo ya msingi ya sekta au taasisi yanakiukwa na hivyo watu kufanya mambo yao kwa vile wanafahamu hakuna msafi katika eneo hilo wa kumkemea mwingine.

Hilo ndilo linaloonekana kwenye TFF ya Tenga kwa sasa, hakuna mtu wa kumfunga mbuzi kengere na kwa vile kila mtu anaingia pale kwa malengo binafsi na sio ya kutufanya Watanzania tuchekelee ushindi kama walivyofanya Nigeria juzi.

Watu wanahakikisha wanaingia TFF hata kwa njia za kiharamia ilimradi tu maslahi yao na marafiki zao yaendelee kulindwa na matokeo yake vijana, ambao wanatakiwa kuandaliwa kwa ajili ya kuliletea sifa taifa kwa soka, wanakosa waongozaji.

Ni wakati sasa wa Watanzania kujiuliza wale vijana waliokwenda Brazil na kufanya vizuri wako wapi? Wale vijana waliokwenda Afrika Kusini na kufanya maajabu wako wapi leo na wanafanya nini? Nani alitakiwa kuwa mlezi wao?

Badala ya kuwalea vijana wale, ambao wangetufuta machozi siku za usoni, watu wana kazi ya kupambana, kuleana na kubebana ili washike madaraka na waje kunufaika na vipaji vya watoto wa Watanzania wenzao.

Lazima sasa Watanzania tuungane kupinga umangimeza huu ambao unaliangamiza soka letu na kulifanya liwe la mdomoni, kwa kuwa watu tunaowapa nafasi wanakuwa kwa ajili ya waliowaweka na marafiki zao.

Huwezi kuandaa mazingira ya mtu awe rais kwa nguvu tena kwa vigezo vya hovyo kabisa, tena vya chuki dhidi ya watu wengine. Mfumo huu unaotaka kujengwa tuupinge kwa nguvu zote.

Tuungane kuupinga hata kama watatufungia kushiriki masuala ya soka. Tuwasute hadharani watu wa aina hii. Tuwaambie kabisa kwamba TFF sio ya mtu bali ya Watanzania. Mchakato wa haki na ushindani wa watu ndio msingi wa kuondoa migogoro na kujenga mshikamano katika soka.

Hatuwezi kukuza soka katikati ya watu kupambana na kuhujumiana. Umoja na nguvu ya pamoja ndio msingi mkubwa katika kukuza soka. Tenga na kundi lake lazima wafahamu kwamba kwenye hili binafsi nitapiga kelele mpaka nikauke koo.

Mwandishi wa makala hii ni msomaji mzuri wa gazeti la Burudani. Anapatikana kwa namba 0713 976894.

No comments:

Post a Comment