KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

DOGO RAMA: MUZIKI UNALIPA


UKITAKA kujua uzuri na ubora wa mwanamuziki, ni pale anapokuwa na uwezo wa kuziba mapengo ya wenzake wanapokuwa wamehama katika bendi ama kukosekana kwa sababu mbalimbali.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwimbaji Ramadhani Athumani 'Dogo Rama' wa bendi ya Twanga Pepeta International baada ya waimbaji zaidi ya wanne wa bendi hiyo kuhama na kujiunga na bendi zingine.

Waimbaji waliohama wakati huo ni Khalid Chokoraa, Kalala Junior na Charles Gabriel 'Baba'. Ilibidi Dogo Rama alazimike kuiga sauti za waimbaji hao kila Twanga Peteta ilipofanya maonyesho yake na mapengo yao hayakuonekana kuwa makubwa.

"Lilikuwa pigo kubwa kwa Twanga Pepeta kwa sababu wanamuziki zaidi ya saba walihama kwa wakati mmoja, wakiwemo waimbaji wa tatu. Lakini hatukubabaika. Nilimtoa wasiwasi mama (Asha Baraka) na kumwambia hakuna kitakachoharibika,"alisema Dogo Rama alipohojiwa na kituo cha redio cha RFA cha mjini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Dogo Rama amekiri kuwa, tangu alipojiunga na Twanga Pepeta, kiwango chake kimuziki kimepanda na kwamba kwa sasa ana uwezo wa kutunga, kuimba, kurapu na kucheza kwa wakati mmoja.

Alisema hakutarajia kupata mapokezi mazuri kutoka katika bendi hiyo, hasa kutokana na ukongwe na ukomavu iliokuwa nao katika muziki. Alisema tangu wakati huo, amekuwa akipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wanamuziki wenzake.

Mbali na kupata mafanikio makubwa kimuziki, Dodo Rama pia amefanikiwa kurekodi albamu yake binafsi, inayokwenda kwa jina la 'Kilometa 10,000'. Amerekodi albamu hiyo kwa kushirikiana na wanamuziki tofauti.

Alisema alipata ruhusa ya kurekodi albamu hiyo kutoka kwa uongozi wa Twanga Pepeta ndio sababu aliweza kushirikiana na baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo katika kurekodi nyimbo zake.

Hata hivyo, Dogo Rama amekiri kukumbana na matatizo mbalimbali, lakini ameweza kukabiliana nayo na kusonga mbele.

"Matatizo yapo karibu katika bendi zote. Uzuri wa nyumba sio rangu, ingia ndani uone. Hakuna binadamu anayeweza kupendwa na wote,"alisema mwanamuziki huyo aliyezaliwa na kukulia mkoani Mwanza.

Dogo Rama ameitaja sababu kubwa, ambazo zimekuwa zikimfanya apate mafanikio kuwa ni pamoja na kufanyakazi kwa kujituma na pia kuipenda kazi yake.

"Napenda kufanyakazi kwa kujituma kwa sababu naipenda. Hata nisipopewa nafasi, sikati tamaa. Ukinibania, usinibanie, mimi ni kazi mtindo mmoja,"alisema.

Ameyataja mafanikio aliyoyapata kutokana na muziki kuwa ni pamoja na kupata pesa za kuendesha maisha yake na pia kumudu gharama zingine muziki kama vile kulipa pango la nyuma na kununua vitu muhimu vya ndani.

Kwa sasa, Dogo Rama ameshaanza maandalizi ya kurekodi albamu yake ya pili na kwamba tayari ameshakamilisha kutunga nyimbo nne. Alisema albamu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni katikati ya mwaka huu.

Amewataja baadhi ya wanamuziki waliomwezesha kufika alipo sasa kuwa ni Benno Villa Antony wa bendi ya Carnival ya mjini Mwanza na marehemu Kyanga Songa.

Dogo Rama alisema pia kuwa, anafurahia kufanyakazi na mwimbaji Luiza Mbutu kwa vile ni mwanamuziki anayependa kujituma na kufanyakazi yake kwa bidii kubwa.

Je, ni kwa nini waimbaji wengi wa bendi za muziki wa dansi hupenda kutaja majina ya watu maarufu katika nyimbo zao?

Akijibu swali hilo, mwanamuziki huyo alisema wanafanya hivyo kwa lengo la kunogesha nyimbo zao na pia wanalipwa na watu hao, ambao wengi ni wafanya biashara.

Dodo Rama amekiri kuwa, tuhuma za uchawi zipo kwa wanamuziki na kwamba baadhi yao wamekuwa wakifanyiana vitendo vya ushirikina kwa lengo la kuharibiana.

Akitoa mfano, alisema kuna wakati aliwahi kupata ajali ya gari katika maeneo ya Sinza baada ya kuona mauzauza ghafla barabarani.

Aliielezea ajali hiyo kuwa, ilitokana na vitendo vya ushirikiana alivyofanyiwa na wapinzani wake kimuziki, lakini walishindwa kufua dafu kwa vile yupo imara.

No comments:

Post a Comment