KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

MALKIA WA NYUKI AWAPONDA VIONGOZI SIMBA NA MAKOCHA WA KIGENI




MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba, Rahma Al-Kharoos ameponda utaratibu wa klabu za Tanzania kuajiri makocha wa kigeni na kuwadharau wazalendo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam jana, Rahma alisema Simba haina hadhi ya kufundishwa na kocha wa kigeni kutokana na viwango walivyonavyo wachezaji.

Rahma alisema viwango vya wachezaji wa Simba ni vya kawaida na amependekeza iwe chini ya Kocha Msaidizi, Jamhuri Kihwelu.

Mwanamama huyo, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Malkia wa Nyuki alisema, kama Simba wanataka kufundishwa na kocha wa kigeni, ni vyema watafute wachezaji wenye viwango vya juu.

Akitoa mfano, alisema ilivyo Simba sasa ni sawa na mtoto wa shule ya awali kufundishwa na mwalimu wa chuo kikuu.

"Kwani sisi hatuna makocha wazalendo, si wapo wengi tu?" Alihoji mwanamama huyo.

Rahma alisema haiingii akilini kuona kuwa, klabu ya Simba inatumia dola 8,000 za Marekani kila mwezi kumlipa mshahara kocha wa kigeni wakati fedha hizo zingeweza kutumika kwa mambo mengine muhimu.

Mfanyabiashara huyo alisema haoni tatizo kwa timu za Tanzania kufundishwa na makocha wazawa kwa sababu katika nchi ya Oman, makocha wa kitanzania wana thamani kubwa.

"Kwa nini tutafute makocha wa nje wakati uwezo wa kuwalipa hatuna. Tunatafuta sifa? Lazima tubadilike,"alisisitiza.

Simba inafundishwa na Kocha Patrick Liewig kutoka Ufaransa, anayesaidiwa na Moses Basena kutoka Uganda na Jamhuri Kihwelu.

No comments:

Post a Comment