LAGOS, Nigeria
MWENYEKITI wa Kampuni za Glo nchini Nigeria, Otunba Mike Adenuga amemzawadia gari na nyumba Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Stephen Keshi.
Otunba amemzawadia Keshi gari aina ya Range Rover Sport, nyumba iliyopo katika Jiji la Lagos na pesa taslim dola 200,000 (sh. milioni 330).
Mfanyabiashara huyo alisema mjini hapa juzi kuwa, ameamua kumzawadia Keshi vitu hivyo kutokana na kuiwezesha Nigeria kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika.
Nigeria ilitwaa taji hilo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuichapa Burkina Faso bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa mjini Johannesburg.
Kikosi cha Nigeria kilirejea mjini Lagos juzi na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wa soka wa jiji hilo. Mapokezi hayo yaliongozwa na viongozi kadhaa wa serikali.
Wakati huo huo, Keshi ameamua kufuta mpango wake wa kujiuzulu kuifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo.
Keshi alitangaza kujiuzulu kuifundisha Nigeria mara baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa kwa kuifunga Burkina Faso.
Nahodha huyo wa zamani wa Nigeria alisema, alifikia uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo (NFF).
Akihojiwa na kituo cha redio cha Metro FM cha Afrika Kusini, Keshi alisema hakufurahishwa na tishio lililotolewa na NFF la kumtimua kazi kabla ya timu hiyo kumenyana na Ivory Coast.
Keshi aliiongoza Nigeria kutwaa taji hilo baada ya miaka 19. Alikuwa nahodha wa kikosi cha Nigeria kilichotwaa taji hilo kwa mara ya mwisho 1994.
Kocha huyo amekuwa mwafrika wa kwanza kuiongoza timu yake kutwaa taji la Mataifa ya Afrika tangi Yeo Martial alipoiwezesha Ivory Coast kutwaa ubingwa 1992.
No comments:
Post a Comment