KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 28, 2013

SIMBA KUIFUATA LIBOLO KESHO



WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa Afrika, Simba wanatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Angola kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Recreativo Libolo.

Simba imepanga kwenda Angola ikiwa na kikosi cha wachezaji 20 na viongozi saba.
Pambano kati ya Simba na Libolo limepangwa kuchezwa Jumapili katika mji mdogo wa Calulo.

Katika mechi ya awali kati ya timu hizo, iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilichapwa bao 1-0. Ili isonge mbele katika michuano hiyo, Simba italazimika kuishinda Libolo mabao 2-1.

Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kikosi kitakachokwenda Angola kinatarajiwa kutangazwa kesho.

Kamwaga alisema wameamua kutokitangaza mapema kikosi hicho kwa kuhofia kujitokeza kwa wachezaji majeruhi katika mazoezi yaliyotarajiwa kufanyika jana na yatakayofanyika leo.

Licha ya kufungwa katika mechi ya kwanza, Kamwaga alisema matumaini ya timu hiyo kusonga mbele ni makubwa kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

"Kufungwa nyumbani haina maana kwamba tumeshatolewa. Mara nyingi hutokea timu kufungwa nyumbani, lakini ikafanya vizuri ugenini,"alisema.

Kamwaga alisema wamepata wasiwasi baada ya kusikia wenyeji wao wamepanga mechi hiyo ichezwe katika mji wa Calulo kwa vile watalazimika kuwasafirisha kwa ndege.

"Hatutakuwa tayari kusafiri kwa basi umbali wa saa nne kwa vile kanuni za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) zipo wazi kuhusu hilo,"alisema.

No comments:

Post a Comment