KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 28, 2013

NIYONZIMA AITAKATISHA YANGA


BAO lililofungwa na Haruna Niyonzima jana liliiwezesha Yanga kujikita zaidi kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Niyonzima alifunga bao hilo dakika ya 65 kwa shuti kali la mbali, ambalo kipa Hannington Kalyesubula wa Kagera Sugar alishindwa kuliona na kujikuta akidaka hewa.

Hii ni mara ya pili kwa Niyonzima kuifungia Yanga bao muhimu katika mechi za ligi kuu ndani ya muda wa siku tano. Wiki iliyopita, Niyonzima aliifungia Yanga bao pekee na la ushindi katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa kwenye uwanja huo.

Ushindi huo uliifanya Yanga iwe na pointi 42 baada ya kucheza mechi 18, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36 na Simba yenye pointi 31.

Pamoja na kupata ushindi, Yanga jana iliweka rekodi baada ya wachezaji wake watano kuonyeshwa kadi za njano. Wachezaji hao ni Saidi Bahanuzi, Athumani Iddi, Nadir Haroub, David Luhende na Nizar Khalfan.

Kutokana na kupata idadi hiyo ya kadi, Yanga inakabiliwa na adhabu ya kutozwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa kanuni za ligi.

Timu zote mbili ziliuanza mchezo huo kwa kasi ndogo, lakini Kagera Sugar walionekana kuchangamka zaidi na kufika kwenye lango la Yanga mara tatu katika dakika za mwanzo.

Yanga ingeweza kufunga bao dakika ya tatu wakati Didier Kavumbagu alipounganisha kwa kichwa krosi ya Simon Msuva, lakini kipa Hannington Kalyesubula alikuwa makini kudaka mpira huo.

Msuva alipata nafasi nzuri ya kuifungia Yanga bao dakika ya 13 baada ya kuunasa mpira uliompita beki Muganyizi Martin ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Hannigton.

Lango la Yanga lilipata msukosuko dakika ya 34 wakati Juma Nade alipofumua shuti kali akiwa umbali wa mita 20, lakini lilipaa juu ya lango.

Dakika nne baadaye, Shija Mkina alipenya na mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga baada ya kupewa pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja, lakini kiki yake ilitoka pembeni ya uwanja.

Yanga ilifanikiwa kupata adhabu ya penalti dakika ya 45 baada ya kipa Hannington wa Kagera kumwangusha Kavumbagu ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la adhabu hiyo la Kavumbagu lilipaa juu ya lango.

Awali, wachezaji wa Kagera waligomea adhabu hiyo kwa madai kuwa, haikuwa halali. lakini waliruhusu ipigwe baada ya kushauriana kwa dakika kadhaa na kushangilia baada ya shuti la Kavumbagu kutoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Yanga ikilianza kipindi cha pili kwa kasi na nusura ipate bao dakika ya 49 wakati Domayo alipofumua shuti kali, lakini liligonga mwamba na mpira kurudi uwanjani, ambako uliokolewa na mabeki wa Kagera.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Athumani Iddi, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu/Jerry Tegete, Saidi Bahanuzi/Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima.

Kagera: Hannington Kalyesubula, Benjamin Asukile, Muganyizi Martin, Malegesi Mwangwa, Amandus Nesta, George Kavilla, Julius Mrope/ Paul Ngwai, Juma Nade, Darlington Enyinna, Shija Mkina, Daudi Jumanne.

No comments:

Post a Comment