'
Friday, February 22, 2013
HASHIM ABDALLA KUZIHUKUMU YANGA NA AZAM
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 23 mwaka huu) kwa mechi tatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yatakuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Uwanja huo wa kisasa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na makamu bingwa Azam. Ingawa Azam imecheza mechi moja zaidi, lakini timu hizo zinatofautishwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwenye msimamo wa ligi huku kila moja ikiwa na pointi 36.
Pia vinara wa ufungaji kwenye ligi kwa sasa wanatoka katika timu hizo mbili. Kipre Tchetche aliyepachika mabao tisa hadi sasa ndiye anayeongoza akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao manane.
Iwapo timu yoyote itafanikiwa kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam, kasi ya mbio za kuwania ubingwa itaongezeka. Waamuzi wasaidizi watakuwa Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam na John Kanyenye kutoka Mbeya wakati mezani atakuwepo Oden Mbaga.
Mechi nyingine za kesho ni Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jumapili (Februari 24 mwaka huu), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa katika hekaheka nyingine kwa Simba chini ya Mfaransa Patrick Liewig kuikabili Mtibwa Sugar inayonolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.
FDL YAENDELEA KUSHIKA KASI
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea wikiendi hii kwa mechi kumi na moja katika viwanja tofauti. Timu hizo zinapambana kutafuta hadhi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao 2013/2014.
Kesho (Februari 23 mwaka huu) kundi A litakuwa na mechi moja itakayozikutanisha timu za Mkamba Rangers na JKT Mlale itakayochezwa Uwanja wa Ruaha mkoani Morogoro.
Kundi B lenyewe litakuwa na mechi mbili; Tessema itacheza na Ashanti United katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam wakati Ndanda itaikaribisha Polisi Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara.
Raundi ya 12 ya ligi hiyo kundi A itashuhudia timu zote nane zikiwa viwanjani; Pamba vs Mwadui (CCM Kirumba), Polisi Tabora vs Polisi Mara (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma vs Morani (Jamhuri) na JKT Kanembwa vs Rhino Rangers (Lake Tanganyika).
Jumapili (Februari 24 mwaka huu) kundi A litakuwa na mechi kati ya Burkina Faso dhidi ya Kurugenzi (Jamhuri), Majimaji vs Polisi Iringa (Majimaji) wakati kundi B ni Transit Camp vs Villa Squad (Karume), na Green Warriors vs Moro United (Mlandizi).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment