KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 3, 2013

SERIKALI YAWAONYA WAGOMBEA TFF


SERIKALI imemtaka rais mpya atakayechaguliwa kuliongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuendeleza mazuri yaliyofanywa na rais anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga.

Mwito huo umetolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana.

Fenella alisema si vizuri kwa rais ajaye wa TFF kujihusisha na migogoro na kusababisha shirikisho hilo lirejee katika matatizo liliyokuwa nayo miaka ya 1990.

Waziri huyo alisema ni vyema rais mpya wa TFF aendeleze yote mazuri yaliyofanywa na Tenga ili kulijengea heshima shirikisho hilo ndani na nje ya nchi.

Uchaguzi mkuu wa TFF unatarajia kufanyika Februali 24, mwaka huu mjini Dar es Salaam. Nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni ya rais, makamu wa rais na wajumbe 13 wa kamati ya utendaji.

Fenella alisema si vyema kwa uongozi mpya wa TFF kubomoa misingi imara ya uongozi na utawala iliyowekwa na Tenga na kuzusha migogoro isiyokuwa na maana.

Alisema migogoro iliyokuwepo awali ndani ya shirikisho hilo kwa sasa imebaki kuwa historia, hivyo si vyema kuwarudisha watu katika kumbukumbu hiyo.

Dk. Fenella alisema kazi kubwa itakayowakabili viongozi wapya wa TFF ni kuzidi kulijenga na kuliimarisha shirikisho hilo badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.

"Uchaguzi wa TFF unakuja na kila mtu anatarajia mambo makubwa zaidi kwa viongozi watakaochaguliwa, hivyo sitarajii kusikia migogoro inarejea, kinachotakiwa hapa ni maendeleo tu," alisema Fenella.

Wagombea wanaowania uongozi katika uchaguzi huo ni Athumani Nyamlani, Jamal Malinzi, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura (rais). Walioomba kuwania nafasi ya makamu wa rais ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.

Wanaogombea ujumbe wa kamati ya utendaji ni Salum Chama na Kaliro Samson (Kagera na Geita), Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii (Arusha na Manyara), Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora).

Wengine ni Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama na Stanley Lugenge (Njombe na Ruvuma), Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida).

Wagombea wengine ni Farid Nahdi, Geofrey Nyange, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majara na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).

No comments:

Post a Comment