'
Thursday, February 28, 2013
TBL YANOGESHA SAFARI YA SIMBA ANGOLA
WATANZANIA wametakiwa kuweka tofauti zao mbali na kuishangilia timu ya Simba inapocheza mechi yake ya marudiano na Libolo ya Angola Jumapili hii kuwania kufuzu katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Wito huo umetolewa na wadhamini wa Timu ya Simba, Kilimanjaro Premium Lager, kupitia Meneja Masoko, Fimbo Butallah wakati wa kutoa vifaa kwa timu ya Simba tayari kwa mechi hiyo kama sehemu ya udhamini.
“Wanapokwenda kwenye mechi hii hawaendi tu kama Simba bali wanakwenda kuiwakilisha Tanzania kwa hivyo ni muhimu kwa watanzania wote kuungana na Kilimanjaro Premium Lager kuleta hamasa ili timu yetu iibuke na ushindi na kusogea mbele katika mashindano haya,” alisema.
Alisema wao kama wadhamini wana imani kuwa Simba imejiandaa vizuri na watafanya maajabu na kuibuka na ushindi ugenini. “Mechi hii ni ngumu, lakini tuna imani watafanya vizuri na kuwafurahisha watanzania,” alisema Butallah.
Akipokea vifaa hivyo, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliishukuru Kilimanjaro Premium Lager kwa udhamini wake mnono, ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa klabu yao.
“Zawadi ambayo tunaweza kuwapa wadhamini wetu ni kushinda Jumapili,” alisema Kamwaga.
Alisema watanzania wasiwe na wasiwasi kwani Simba ina uwezo wa kufanya ilichofanya kwa Zamalek miaka kumi iliyopia kwani Zamalek ilishinda Tanzania lakini katika mechi ya marudiano Simba ikashinda.
“Kuna wakati pia Mufurira Wanderers ya Zambia ilitufunga mabao manne nyumbani lakini tulivyoenda kwa tukawafunga matano,” alisema Kamwaga.
Simba inatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kwenda Angola kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumapili.
Kilimanjaro Premium Lager ni mdhamini wa timu za Simba na Yanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment