KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 2, 2012

TIKETI ZA PAMBANO LA SIMBA NA YANGA ZAGOMBEWA KAMA NJUGU


Tiketi kwa ajili ya mechi ya Yanga na Simba itakayochezwa keshokutwa (Oktoba 3 mwaka huu) zimeanza kuuzwa leo kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo namba 8 ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa moja kamili usiku.
Vituo vinakavyotumia kuuza tiketi hizo kuanzia saa 4 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja wa Taifa, Kituo cha Mafuta OilCom Ubungo, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio/Samora, Dar Live Mbagala na Kituo cha Mafuta Buguruni.
Mwandishi wa blogu hii aliyetembelea vituo hivyo leo, alishuhudia mashabiki kibao wakigombea kununua tiketi hizo huku katika baadhi ya maeneo, tiketi za sh. 5,000 zikiripotiwa kumalizika mapema.
Kiingilio cha chini kwenye mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000. Watazamaji watakaoketi kwenye viti vya rangi ya bluu ambavyo ni 17,045 watalipa sh. 7,000 kwa tiketi moja.
Sh. 10,000 ni kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 wakati VIP C inayochukua watazamaji 4,060 itakuwa sh. 15,000. Kwa upande wa VIP B tiketi ni sh. 20,000 na VIP A yenye watazamaji 748 tu kiingilio kitakuwa sh. 30,000.
Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza, akisaidiwa na Samuel Mpenzu kutoka Arusha na Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam wakati mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment