'
Saturday, October 27, 2012
SIMBA YAITOA NISHAI AZAM, YANGA YAPAA
SIMBA jana iling'ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Azam mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda ndiye aliyeing'arisha Simba baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Bao lingine lilifungwa na Felix Sunzu.
Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake nyota, John Bocco, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia dakika ya 20.
Ushindi huo uliiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 10, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 20 na Azam yenye pointi 18.
Yanga ilichupa nafasi ya pili baada ya jana kuichapa JKT Oljoro bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Bao pekee na la ushindi la Yanga lilifungwa na beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, African Lyon ilitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Ruvu Shooting iliichapa Polisi Morogoro mabao 2-1 kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment