KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 18, 2012

SIMBA YAVUTWA SHARUBU




SIMBA jana ililazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Kagera Sugar katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Licha ya kulazimishwa sare, Simba bado inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 17, JKT Oljoro yenye pointi 13 na Kagera Sugar yenye pointi 12.
Simba itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani iliweza kuongoza mabao 2-0 hadi dakika ya 61 wakati Kagera ilipopata bao na hatimaye kusawazisha.
Kagera ililianza pambano hilo kwa kasi na kupata kona dakika ya kwanza, lakini haikuwa na madhara yoyote kwenye lango la Simba.
Simba ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya saba wakati Felix Sunzu alipojitwisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Nassoro Masoud kutoka pembeni ya uwanja, lakini uliokolewa na kipa Andrew Ntalla wa Kagera.
Sunzu alisahihisha makosa dakika ya nane baada ya kuifungia Simba bao kwa kichwa, kufuatia krosi maridhawa iliyopigwa na Mrisho Ngasa.
Daudi Jumanne nusura aipatie bao Kagera dakika ya 25 baada ya kumtoka Amri Kiemba wa Simba na kufumua shuti kali, lakini lilitoka pembeni ya lango.
Haruna Moshi aliikosesha Simba nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 32 alipobaki ana kwa ana na kipa Ntalla, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Emmanuel Okwi, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kagera ilipata bao la kwanza kupitia kwa Themi Felix kabla ya Salum Kanoni kuisawazishia kwa njia ya penalti baada ya beki Nassoro Masoud kumwangusha Paul Ngwai ndani ya eneo la hatari.
SIMBA: Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Juma Nyoso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa.
KAGERA SUGAR: Andrew Ntalla, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus Nesta, Benjamin Effe, Malagesi Mwangwa, Daudi Jumanne, George Kavilla, Shija Mkina, Enyima Darlington, Wilfred Ammeh.

No comments:

Post a Comment