MCHEZA filamu nyota wa kike wa Nigeria, Omotola Jalade amesema fani hiyo inaweza kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo kuliko Marekani.
Omotola alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Focus on Africa kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha BBC.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema, kwa sasa Wanigeria (Nollywood) wamepiga hatua kubwa katika fani ya filamu na wanakaribia kuwapiku Wamarekani (Hollywood).
Alisema hilo linatokana na kiwango cha filamu za Kinigeria kuwa juu na kukubalika na mashabiki wengi katika sehemu mbali mbali duniani.
Omotola alisema kwa sasa, filamu za Kinigeria zinaweza kuingia kwenye ushindani na zile za Hollywood.
Mwanadada huyo, ambaye ni mama wa watoto wanne, aliwekuwepo mjini London kwa ajili ya uzinduzi wa filamu yake mpya, inayojulikana kwa jina la Amina.
Uzinduzi wa filamu hiyo ulihudhuriwa na wasanii mbali mbali wa fani hiyo kutoka barani Afrika na Ulaya na kuwa na mvuto wa aina yake.
Mara baada ya kuteremka kwenye gari karibu na eneo la uzinduzi, Omotola alitembea kwenye zulia jekundu hadi ukumbini, ambako filamu hiyo ilionyeshwa kwa wageni mbali mbali.
Omotola alikuwa kivutio kikubwa kwa wageni hao kutokana na kuvalia gauni lenye thamani kubwa, lililonakshiwa kwa vitu mbali mbali vya kumeremeta na kumfanya aonekane kama vile malkia.
Baadhi ya mapaparazi waliohudhuria uzinduzi huo walikuwa wakihaha kupata picha za mwanadada huyo, ambaye hakuwa na hiyana zaidi ya kuwapa pozi za aina mbali mbali.
Omotola amecheza filamu hiyo akiwa mwigizaji mkuu. Filamu hiyo imemwezesha kushinda tuzo ya BEFFTA.
No comments:
Post a Comment