UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuwaongeza makamu mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Davis Mosha na Abdul Sauko kwenye kamati ya mashindano kwa ajili ya kuongeza nguvu.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, uamuzi wa kuwaongeza Mosha na Sauko kwenye kamati hiyo,ulifikiwa hivi karibuni kwenye kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo.
Katika kikao hicho, wajumbe waliafiki kwa kauli moja kuongezwa kwa Mosha na Sauko kwenye kamati hiyo kutokana na uzoefu wao katika uongozi wa soka na kusimamia timu.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ameieleza Burudani kuwa, kamati hiyo kwa sasa imepwaya kutokana na kutokuwa na wapiganaji wenye uwezo wa kupambana na timu pinzani.
"Tumeona wajumbe wengi waliopo sasa kwenye kamati hiyo hawafahamu vyema fitina za soka kama walivyo Mosha na Sauko,"alisema mjumbe huyo.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji anatarajia kuwatangaza rasmi wajumbe hao wapya baada ya kurejea nchini kutoka Makka, ambako amekwenda kwa ajili ya ibada ya hija.
Katika hatua nyingine, kuchelewa kurejea nchini kwa mshambuliaji, Hamisi Kiiza wa Yanga kumezusha hali ya wasiwasi katika benchi la ufundi la timu hiyo.
Kiiza alikwenda Uganda kwa ajili ya kuichezea timu hiyo katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2013 zitakazofanyika Afrika Kusini.
Katika mechi hiyo dhidi ya Zambia iliyopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Kampala, Uganda ilitolewa kwa mikwaju ya penalti baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Habari kutoka katika benchi la ufundi la Yanga zilieleza jana kuwa, Kiiza ilikuwa arejee nchini juzi, lakini alishindwa kutokana
na kuuguliwa na mtoto wake.
Kwa mujibu wa habari hizo, mchezaji huyo sasa anatarajiwa kurejea nchini leo kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi ya ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting, itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment