KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 10, 2012

YANGA WANAWEWESEKA-RAGE



MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ameiponda klabu ya Yanga kwa madai kuwa, imeanza kuweweseka kutokana na kupoteza mechi nyingi za ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Rage alisema kiwewe hicho ndicho kimewafanya viongozi wa Yanga waituhumu Simba kwamba imetia mkono katika mechi walizofungwa.
Rage alisema kuvurunda kwa Yanga katika ligi kuu ya msimu huu kumetokana na viongozi wake kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kulipwa malimbikizo ya madeni wanayodaiwa.
Hadi sasa, Yanga imepoteza mechi mbili za ligi hiyo kwa kuchapwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro kabla ya kupigwa mweleka wa bao 1-0 na Kagera Sugar mjini Bukoba. Pia wamelazimishwa kutoka suluhu na Prisons mjini Mbeya.
Mechi pekee walizoshinda ni dhidi ya JKT Ruvu, ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na dhidi ya African Lyon, ambayo waliichapa mabao 3-1. Mechi zote hizo zilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga inatarajiwa kucheza mechi nyingine leo kwa kumenyana na ndugu zao wa Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
"Hawa ndugu zetu wamefungwa mechi nyingi na sasa wamelewa mabao, wanasahau hata kulipa pesa wanazodaiwa," alisema Rage.
Yanga wanadaiwa mamilioni ya pesa, ikiwa ni malimbikizo ya malipo ya mchezaji John Njoroge wa Kenya na Kocha Kostadin Papic kutoka Serbia. Pia wanadaiwa dola 32,000 za Marekani (sh. milioni 34), ambazo Simba ilimlipa beki Mbuyu Twite kwa ajili ya usajili wa msimu huu kabla ya mchezaji huyo kuhamia Yanga.
Wakati huo huo, klabu ya Yanga imekiri kutoilipa Simba fedha ilizotoa kwa ajili ya usajili wa beki Mbuyu Twite kutoka Rwanda.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshindwa kulipa pesa hizo kutokana na matatizo mbali mbali, lakini hakutaka kufafanua zaidi.

No comments:

Post a Comment